KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Wednesday, August 18, 2010

NASRI NJE MWEZI MMOJA.


Kikosi cha washika bunduki wa Ashberton Grove Arsenal kimeendelea kumeng’enyuka baada ya hii leo kuthibitika huenda kikamsa kiungo wake wa kimataifa toka nchini Ufaransa Samir Nasri kwa muda wa mwezi mmoja.

Kiungo huyo hatokuwepo kikosini kwa muda huo kufuatia kuwa na maumivu ya goti aliyoyapata kwenye mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Liverpool uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bao moja kwa moja.

Taarifa toka ndani ya klabu hiyo ya jijini London imeeleza kuwa, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 huenda akafanyiwa upasuaji mdogo ambao utamkosesha michezo mitano mfululizo.

Kuumia kwa Samir Nasri, kunamfanya ajiunge na wachezaji wenzake kama Alex Song, Denilson, Aaron Ramsey pamoja na Johan Djourou ambao nao ni majeruhi.

Hata hivyo tayari imeshaelezwa kuwa huenda nafasi ya Samir Nasri ikajazwa na kiungo Jack Wilshire kwa kusaidiana na Cesc Fabregas anaetarajiwa kurejea katika mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Blackpool utakaochezwa mwishoni mwa juma hili mwenye uwanja wa Emirates.

No comments:

Post a Comment