KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Monday, June 13, 2011

KIVUMBI CHA KOMBE LA SHIRIKISHO 2010-11.


Michuano ya kombe la shirikisho la soka barani Afrika CAF, ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua ya mtoano, mwishoni mwa juma lililopita imeendelea tena katika viwanja kadha wa kadha barani humo huku klabu ya JS Kabylie ya nchini Algeria ikiwa ya kwanza kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kuichapa klabu ya ASC Jaraaf ya nchini Senegal mabao mawili kwa sifuri.

Mabao ya JS Kabylie yalipachikwa wavuni na beki Chemseddine Nessakh pamoja na kiungo Saad Tedjar hatua ambayo imeifanya klabu hiyo iliyowahi kutwaa ubingwa wa barani Afrika mwaka 1981 na 1990 kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1.

Nayo klabu ya Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast imesonga mbele baada ya kulazimisha matokeo ya sare bao moja kwa moja ugenini dhidi ya Primeiro Agosto ya nchini Angola na hivyo kupata ushindi wa jumla ya mabao matano kwa moja kufuatia ushindi wa mabao manne kwa sifuri uliopatikana kwenye mchezo wa kwanza uliounguruma mjini Abidjan.

Klabu nyingine kutoka nchini Angola Inter Clube yenyewe imefanikiwa kupenya na kutinga katika hatua ya makundi kufuatia sare ya mabao mawili kwa mawili iliyopatikana ugenini dhidi ya klabu ya Difaa al Jadida ya nchini Morocco, ambapo katika mchezo wa kwanza Difaa al Jadida alikubali kisago cha mabao matatu kwa sifuri.

Klabu ya Kaduna utd ya nchini Nigeria nayo imefanikiwa kutinga katika hatua ya makundi baada ya kupata ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya klabu ya Entente Setif ya nchini Algeria.

Katika mchezo wa kwanza Kaduna Utd walipoteza kwa kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.

Klabu ya Simba ya Tanzania nayo imeingiza mguu mmoja ndani ya mduara wa hatua ya makundi kufuatia ushindi wa bao moja kwa sifuri ulipatikana jana dhidi ya Dc Motema Pembe, na huenda ikaingiza miguu yote miwili endapo itapata matokeo mazuri katika mchezo wa pili utakaofanyika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

No comments:

Post a Comment