KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Tuesday, June 7, 2011

Martin Jol AREJEA JIJINI LONDON !!


Hatimae aliekua meneja wa Tottenham Hotspurs Martin Jol amerejea tena katika ligi kuu ya soka nchini Uingereza kufuatia uongozi wa klabu ya Fulham kumsainisha mkataba wa miaka miwili huko Craven cottage.

Martin Jol ameingia mkataba na klabu ya Fulham kufuatia kuondoka kwa aliekua meneja klabuni hapo Mark Hughes, ambae aliamua kufungasha kilicho chake kati kati ya juma lililopita huku akiendelea kuhusishwa na taarifa za kutaka kujiunga na klabu ya Aston Villa.

Makubaliano ya meneja huyo wa kidachi ya kusaini mkataba wa kukinoa kikosi cha klabu ya Fulham yamefikiwa hii leo huko jijini London chini ya mmiliki wa The Cottegers Mohamed Al Fayed.

Akizungumza kupitai mtandao wa klabu ya Fulham Martin Jol amesema ni furaha sana kwake kurejea jijini London tena kwenye klabu yenye msingi na utamaduni mzuri wa ushindani hatua ambayo anaamini itamuwezesha kufanya kazi kwa uhuru.

Amesema anachofikiria kwa sasa mara baada ya kusaini mkataba wa kukinoa kikosi cha klabu hiyo ni mikakati iliyo thabiti ambayo itamuwezesha yeye pamoja na timu nzima kwa ujumla kufikia malengo yaliyowekwa kwa ajili ya msimu wa mwaka 2011-12.

Msimu uliopita wakati Roy Hodgson akiondoka Craven Cottage na kujiunga na Liverpool, Martin Jol alikua kwenye orodha ya mameneja waliokua wakipigiwa upatu wa kujiunga na klabu hiyo lakini dakika za mwisho uongozi uliamua kuingia mkataba na Mark Hughes.

Martin Jol aliondoka nchini Uingereza mwaka 2007, baada ya kutimuliwa kazi huko White Hart lane yalipo makao makuu ya Spurs baada ya mambo kumuendea kombo mwanzoni mwa msimu wa mwaka 2006-07.

Akiwa klabuni hapo kuanzia mwaka 2004, alianza kama meneja msaidizi ambapo bosi wake alikua Jacques Santini, kutoka nchini Ufaransa na alipandishwa cheo mara baada ya kuondoka kwa bosi wake.

Baada ya kuondoka nchini Uingereza mwaka 2007 Martin Jol alijiunga na klabu ya Hamburg ya nchini Ujerumani mwezi July 2008 ambapo huko alidumu kwa msimu mmoja kabla ya kurejea nyumbani kwao Uholanzi kukinoa kikosi cha Ajax Amsterdam na mwezi Novemba mwaka 2010 aliamua kuachana na klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment