KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Friday, July 22, 2011

TORRES AENDELEA KUPEWA MUDA ZAIDI.


Siku moja baada ya ushindi wa bao moja kwa sifuri uliopatikana katika mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya kikosi maalum cha nchini Malaysia, meneja wa klabu ya Chelsea Andre Villas-Boas amkingia kifua mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Hispania Fernando Torres.

Andre Villas-Boas amejitoa muhanga kumkingia kifua mshambuliaji huyo kufuatia ukame wa kupachika mabao unaendelea kumtawala toka aliposajiliwa na Chelsea mwezi januari akitokea Liverpool ambapo mpaka sasa ameshafanikiwa kuifungia klabu hiyo ya jijini London bao moja katika michezo kumi na nne aliyocheza.

Lawama kwa Fernando Torres ziliibuka tena mara baada ya mchezo wa jana huko mjini Kuala Limper kufuatia kukosa nafasi kadha wa kadha za kupachika mabao ambazo zingeisaidia Chelsea kuibuka na ushindi wa mabao mengi zaidi ya bao moja lililofungwa na Didier Drogba.

Andre Villas-Boas amesema anachokihitaji yeye ni ushindi na wala hatotazama nani amefunga bao tena kwa kigezo cha thamani ya usajili wa mchezaji ilioyompeleka Stamford Bridge.

Hata hivyo amedai kwamba bado kuna wigo mpana wa michezo ya ligi ya msimu ujao hivyo anashangazwa na baadhi ya mashabiki kumtathmini mchezaji mmoja baada ya mwingine kupitia michezo ya maandalizi ambayo anaitumia kama sehemu ya kurekebisha makosa yanayoonekana.

Chelsea watarejea tena uwanjani kucheza mchezo mwingine wa maandalizi ya msimu ujao wa ligi siku ya jumapili kwa kupambana na kikosi maalum cha nchini Thailand, na kisha wataelekea nchini China katika mji wa Hong Kong kushiriki michuano ya Barclays Asia Trophy itakayozijumuisha klabu za Blackburn Rovers, Aston Villa pamoja na Kitchee Fc .

No comments:

Post a Comment