KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Wednesday, July 20, 2011

UMRI SIO TATIZO KWANGU - Shay Given



Kipa wa kimataifa toka jamuhuri ya Ireland Shay Given amesema suala la umri sio tatizo kwake na bado ataendelea kuutumikia mchezo wa soka kama matarajio yake alivyoyapanga.

Shay Given mwenye umri wa miaka 35, ametoa msimamo huo akiwa katika mkutano wa kutambulishwa kwa waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha usajili na klabu ya Aston Villa akitoke Man City.

Amesema umri wake bado unamruhusu kucheza soka na unaendelea kumpa hali ya kujiamini zaidi anapokua langoni na ndio maana amekua hakatishwi tamaa pale anapopata changamoto akiwa katika majukumu yake ya kikazi.

Hata hivyo Shay Given aliekubali kusaini mkataba wa miaka mitano ya kuitumikia Aston Villa amewataka mashabiki wanaombeza kwa kigezo cha umri wake, kuchulia mfano wa kipa aliekuwepo klabuni hapo Brad Friedel ambae amejiunga na Tottenham Hotsopurs kwa mkataba wa miaka miwili.

Amesema kipa huyo kutoka nchini Marekani ana umri wa miaka 40, na kila leo amekua akijituma huku kila shabiki ulimwenguni akikubali mchango wake alioutoa akiwa na Aston Villa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita .

Kipa mwingine aliemtumia kama sehemu ya kumfananisha na yeye kwa kigezo cha umri ni Edwin Van der sar ambae alitangaza kustahafu mwishoni mwa msimu uliopita akiwa na umri wa miaka 40.

Shay Given pia akazungumzia hatua ya kuondoka kwake Man city kwa kusema isichukuliwa kama ana uhasama na kipa chipukizi Joe Hart ama viongozi wa klabu hiyo bali amefanya maamzui binafsi yanayostahili kuheshimiwa na kila mmoja ulimwenguni.

Alex McLeish meneja alipewa jukumu la kushika pahala palipoachwa wazi na Gerrard Houllier mwishoni mwezi uliopita amesema kusajiliwa kwa kipa huyo kunafungua milango mingine zaidi ya kutimiza malengo ya kufanya usajili wa wachezaji waliosalia kwenye orodha yake.

Katika hatua nyingine Alex McLeish amezungumzia dili la usajili wa mshambuliaji wa pembeni wa Wigan Atheltics Charles N'Zogbia ambapo amesema katu hawezi kulipa zaidi ya paund million 9 kama ada ya uhamisho wa mchezaji huyo aliekuwa kinara wa kuiwezesha The Latics kusalia kwenye ligi kuu mwishoni mwa msimu uliopita.


Amesema endapo uongozi wa Wigan utaendelea na msimamo wake wa kutaka kumuuza mchezaji huyo kwa zaidi ya ofa waliyoituma majuma mawili yaliyopita huko DW Stadium, yu radhi kuvunja dili hilo na kuendelea na usajili wa wachezaji wengine.

Wakati meneja huyo aliepokelewa kwa zogo kubwa na mashabiki wa Aston Villa mara baada ya kuthibitika amesaini mkataba wa kukinoa kikosi chao akitokea Birmingham City akilitema dili la kumsajili Charles N'Zogbia, beki wa klabu ya Sunderland Titus Bramble amesema ana matumaini klabu hiyo itafanikiwa kumnasa winga huyo kutoka nchini Ufaransa.

Titus Bramble ametangaza tambo hizo baada ya ofa ya klabu ya Sunderland kukataliwa na uongozi wa Wigan Atheltics ambao umeendelea kudai kiasi kikubwa cha fedha kama ada ya usajili wa Charles N'Zogbia.

Amesema pamoja na kukataliwa kwa ofa hiyo anaamini viongozi wa pande zote mbili watarejea mezani na kupata muafaka wa kumuhamisha mchezaji huyo kutoka DW Stadium mpaka Stadium Of Light kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili August 31.

Titus Bramble aliwahi kucheza na Charles N'Zogbia wakiwa na kikosi cha Newcastle Utd kabla ya kila mmoja kutimka huko St James Park.

No comments:

Post a Comment