KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Wednesday, August 17, 2011

ARSENE WENGER MATATIZONI !!


Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger huenda akaadhibiwa na shirikisho la soka barani ulaya UEFA kufautia kitendo cha kufanya mawasiliano ya njia ya simu na benchi la ufundi la klabu hiyo wakati wa mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano dhidi ya klabu ya Udinese ya nchini Italia uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo jijini London nchini Uingereza.

Arsene Wenger anafikiriwa kuingia katika kadhia hiyo huku akiwa amemaliza adhabu aliyopewa na UEFA ya kukaa jukwaani katika mchezo mmoja wa michuano iliyo chini ya shirikisho hilo ambapo jana alifanya hivyo kwa masikitiko makubwa.

Mara kadhaa mzee huyo kutoka nchini Ufaransa alionekana katika picha za televisheni akitoa maagizo kwa kocha wa kikosi cha kwanza cha Arsenal Boro Primorac ambae alikua nae jukwaani na kisha alionekana kutokutulia.

Hatua hiyo inatafsiriwa kuwa Arsene Wenger alikaidi maagizo ya UEFA ya kutotakiwa kujishughulisha na masuala yoyote ya benchi la ufundi ikiwa kama sehemu ya adhabu aliyopewa na sasa huenda akaangia tena kikaangoni.

Arsene Wenger aliadhibiwa na kamati ya maadili ya shirikisho la soka barani ulaya UEFA, baada ya kumsemea maneno makali muamuzi kutoka nchini Uswiz Massimo Busacca, mara baada ya mchezo wa hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa, msimu uliopita dhidi ya Barcelona ambapo Arsenal waliondolewa kwa jumla ya mabao manne kwa matatu.

Katika mchezo wa jana Arsenal waliibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri lililopachikwa kimiani na winga kutoka nchini Uingereza Theo Walcott katika dakika ya nne.

Mchezaji wa zamani wa Arsenal David O'Leary ambae pia aliwahi kuvinoa vikosi vya klabu za Leeds Utd, Aston Villa pamoja na Club Al-Ahli ya falme za kiarabu ameuzungumzia mchezo huo kwa kusema Arsena bado wana kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa pili utakaochezwa juma lijalo nchini Italia.

Amesema Arsenal walistahili kumaliza shughuli hiyo mapema kwa kupata mabao zaidi ya mawili lakini udhaifu wa kikosi kilichopangwa jana ulisababisha klabu hiyo kuchomoza na ushindi mwembamba na bao moja kwa sifuri huku akimwagia sifa kede kede mlinda mlango Wojciech Szczęsny.

No comments:

Post a Comment