KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Friday, August 12, 2011

SAKARTA LA USAJILI NA KLABU YA ARSENAL.


Hali ya sintofahamu juu ya safari ya kuuzwa kwa viungo wa klabu ya Arsenal Cesc Fabregas pamoja na Samir Nasri imeendelea kushamiri, kufuatia wachezaji hao kuenguliwa kwenye kikosi kitakachocheza mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza dhidi ya Newcastle Utd hapo kesho.

Wachezaji hao kwa muda sasa wamekua wakihusishwa na taarifa za kutaka kuondoka huko Emirates Stadium, hatua ambayo imeonekana kumvuruga meneja wa Arsenal Arsene Wenger ambae ana deni kubwa la kutwaa vikombe mbele ya mashabiki wa The Gunners.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliokua na lengo la kueleza maandalizi ya kuelekea katika mchezo wa kesho dhidi ya Newcastle Utd, Arsene Wenger amesema kuachwa kwa wachezaji hao nje ya kikosi hakumaanishi kuruhusiwa klabuni hapo na kujiunga na vilabu vinavyowahitaji.

Amesema wachezaji hao amewapumzisha kwa ajili ya kuwapa muda wa kujiandaa vyema, hasa ikizingatiwa Cesc Fabregas anaewaniwa na FC Barcelona alikua majeruhi na Samir Nasri anaewaniwa na Man City ametoka kwenye majukumu ya kitaifa baada kujumuishwa katika kikosi cha Ufaransa kilicholazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Chile siku mbili zilizopita.

Katika hatua nyingine Arsene Wenger amekataa kata kata kuzungumzia suala la uhamisho wa Samir Nasri kwa kusema suala hilo halipo kichwani kwake kwa sasa zaidi ya kufikiria mchezo wa kesho dhidi ya Newcastle Utd.

Amesema kikubwa kilicho mbele yao ni mchezo wa ligi ambao ni muhimu katika suala la kusaka point tatu na kama kuna yoyote anaemuhitaji Samir Nasri anatakiwa kufuata taratibu zinazofahamika.

Saa chache mara baada ya kumalizika kwa mkutano na waandishi wa habari, chombo kimoja cha nchini Hispania kiliripoti taarifa za nahodha na kiungo wa klabu ya Arsenal kukamilisha dili la kujiunga na FC Barcelona.

Catalan daily Sport, wameripoti kwamba Cesc Fabregas hii leo mchana alikua njiani kuelekea mjini Barcelona kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya baada ya viongozi wa pande hizo mbili kukubaliana dili la paund million 27, kama ada ya uhamisho wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24.

Dili la kuuzwa kwa Fabregas lilikuwa ni paund million 30, lakini mazungumzo yaliyojiri kwa siku kadhaa yalisababisha viongozi wa Arsenal kukubali kiasi cha paund million 27 baada ya kuombwa kupunguza kiasi hicho cha fedha.

Catalan daily Sport pia wamethibitisha kwamba Cesc Fabregas, atakapofanyiwa vipimo na ikathibitisha anakidhi vigezo vinavyotakiwa huko camp Nou, atasaini mkataba wa miaka mitano wa kuichezea klabu ya Barcelona ambayo ilimkuza kabla ya kuondoka akiwa na umri wa miaka 16.

No comments:

Post a Comment