KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Saturday, September 17, 2011

ARSENAL WAMNUSURU STEVE KEAN.

Hatimae meneja wa Blackburn Rovers Steve Kean amepata nafasi ya kupumua kufuatia hii leo kikosi chake kuchomoza na ushindi wa kwanza katika michuano ya ligi kuu ya soka nchini Uingereza dhidi ya Arsenal waliokubali kisago cha mabao manne kwa matatu.

Kabla ya mchezo huo mashabiki wa rovers tayari walikua wameshatoa tahadhari kwa uongozi wa klabu hiyo ambayo ilieleza wazi namna wasivyopendezwa na mwenendo wa meneja Steve Kean toka msimu huu ulipoanza August 13.

Meneja huyo kutoka nchini Scotland, hii leo alionekana kuwa na hali ya kujiamini zaidi hatua ambayo inaaminika huenda ilitoa msukumo kwa wachezaji wake kucheza kwa kujituma wakati wote dhidi ya Arsenal ambao wamekua na mwendo wa kusua sua.

Katika mchezo huo Arsenal walionyesha uwezo mkubwa katika kipindi cha kwanza na kupelekea kupata mabao mawili yaliyofungwa na winga kutoka nchini Ivory coast Gervas Gao Gervinho pamoja na kiungo kutoka nchini Hispania Mikel Arteta, huku mshambuliaji kutoka nchini Nigeria Yakubu Aygbein akifunga bao la kwanza kwa upande wa Balckburn Rovers.

Kipindi cha pili Blackburn Rovers walionyesha uwezo mkubwa na wa kushangaza pale walipomiliki mpira kwa kiwango cha hali ya juu, hatua iliyopelekea kupata bao la kusawazisha ambalo lililotokana na kiungo wa Arsenal Alex Song kujifunga mwenyewe.

Bao la tatu likafungwa Yakubu Aygbein na bao la nne lilitokana na beki wa Arsenal Laurent Koscielny kujifungwa mwenyewe huku bao la tatu la The Gunners likipachikwa wavuni na mshambuliaji kutoka nchini Morocco Marouane Chamakh.

Mara baada ya mchezo huo Steve Kean alivieleza vyombo vya habari kwamba ni faraja kubwa kwake pamoja na timu nzima ya benchi la ufundi na pia anaamini ushindi walioupata hii leo ni njia nzuri ya kusaka mafanikio zaidi katika michezo ya ligi inayofuata.

Arsene Wenger meneja wa klabu ya Arsenal yeye aliwaeleza waandishi wa habari juu ya masikitiko yake kwa kusema haukua mchana mzuri kwake kutokana na muonekano wa mchezo ulivyokua hasa ikizingatiwa walikua wakiongoza mabao mawili kwa moja hadi wakati wa mapumziko.

Mzee huyo ameendelea kuamini kwamba bado kikosi chake kinaendelea kutengemaa na kwa sasa anatazama mchezo ujo ambapo watakutana na Shrewsbury Town katika michuano ya kombe la ligi siku ya jumanne ya juma lijalo.

Michezo mingine ya ligi kuu ya soka nchini uingereza iliyochezwa hii leo ni pamoja na.


Goodison Park, Liverpool
Everton 3 - 1 Wigan Athletic

Reebok Stadium, Bolton
Bolton Wanderers 1 - 2 Norwich City

Villa Park, Birmingham
Aston Villa 1 - 1 Newcastle United

The Liberty Stadium, Swansea
Swansea City 3 - 0 West Bromwich Albion

Molineux, Wolverhampton
Wolverhampton Wanderers 0 - 3 QPR

No comments:

Post a Comment