KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Wednesday, September 14, 2011

UCHUNGUZI DHIDI YA TORRES UMEFUTWA - AVB.

Ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Bayer Leverkusen umekua kichocheo kikubwa cha kufuta mipango ya kufanyika uchunguzi wa kina dhidi ya mshambuliaji kutoka nchini Hispania Fernando Torres ambae mwishoni mwa juma lililopita alitoa kauli ya kuwakashifu wachezaji wenzake huko Stamford Bridge.

Taarifa za kufutwa kwa muendelezo wa uchunguzi huo zimethibitishwa na meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas mara baada ya mpambano wa usiku wa kuamkia hii leo ambapo The Blues walianza vyema kwa kupata point tatu ambazo zinawaweka kileleni mwa kundi la tano.

Andre Villas-Boas amesema hakuna haja ya kuendelea na uchunguzi dhidi ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, kutokana na kile alichokifanya katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mashabiki lukuki huko Stamford Bridge.

Amesema Fernando Torres anastahili sifa za kipee kutokana na mchango mkubwa alioutoa kikosini, hatua ambayo ilipelekea kuchangia vionjo vilivyosababisha upatikanani wa mabao mawili ya ushindi yaliyofungwa na kiungo kutoka nchini Hispania Juan Mata pamoja na beki kutoka nchini Brazil David Luiz.

Katika hatua nyingine meneja huyo kutoka nchini Ureno ameonyesha kuwa na shauku ya kukutana na mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza Man utd mwishoni mwa juma hili kufuatia chachu ya ushindi iliyopatikana dhidi ya Bayer Leverkusen.

Amesema kikosi chake kipo vizuri na haofii lolote dhidi ya Man utd ambao toka msimu huu ulipoanza wameonyesha uwezo mkubwa wa kuwabamiza wapinzani kwa idadi kubwa ya mabao.

Katika hatua nyingine kipa wa klabu hiyo ya jijini London Petr Čech ameungana na Andre Villas Boas kwa kusema matokeo ya mabao mawili kwa sifuri ni mazuri kwao na yatawajengea uwezo wa kujiamini zaidi katika michezo ijayo wakianza na mchezo dhidi ya mashetani wekundu.

Amesema hakuna wanalolihofia kwa sasa zaidi ya kuendelea kuhimizana kufanya vyema wao kama wachezaji na wanaamini kila kitu kinawezekana hadi mwishoni mwa msimu huu.

No comments:

Post a Comment