KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Tuesday, December 28, 2010

NILIJUA WANAKWENDA KUFANYA NINI UWANJANI.


Mkuu wa jeshi la Ashburton Grove Arsene Wenger amesema alitambua nini wachezaji wake wanakwenda kukifanya kwenye mchezo wa jana dhidi ya Chelsea ambao waliifunga safari kutoka magharibi hadi kaskazini mwa jiji la London.

Wenger ameyazungumza hayo saa chache mara baada ya pambano hilo kumalizika ambapo kikosi chake kilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja ambao sasa umewarejesha kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi.

Amesema suala kubwa ambalo lilimpa matumaini ya kujua nini wachezaji wake wanakwenda kukifanya uwanjani hiyo jana ni ukomavu wa kiakili na kimwili ambao wameuonyesha toka mwanzoni mwa msimu huu ambapo wamepania kurejesha hadhi ya klabu ya Arsenal kwa kuhakikisha wanatoa ushindani wa kutosha wa kutwaa ubingwa.

Mzee huyo wa kifaransa amebainisha kwamba kikosi chake kilichofanikisha lengo la ushindi ndio kikosi kilichoshinda kwa mara ya mwisho kilipocheza na Chelsea mwaka 2008 hivyo haikumshutua kukirejesha tena uwanjani kupambana na mabingwa hao watetezi.

Akizungumzia mchezo mzima kwa ujumla Wenger ametanabai kwamba katika dakika za mwanzoni kila upande ulicheza kwa kujihami licha ya wachezaji wake kuonyesha uchu wa kufika langoni mwa wapinzani wao, lakini hatua ya kuelekea mapumziko wakiwa wanaongoza ilikua ni faida kubwa sana kwa kikosi chake.

Wakati Arsene Wenger akitamba kujua nini wachezaji wake walikwenda kukifanya uwanjani usiku wa kuamkia hii leo, mpinzani wake Carlo Ancelotti ametoa wito kwa wachezaji wake kuhakikisha wanaamka usingizini na kurejea kwenye hali yao ya kawaida kama ilivyokua mwanzoni mwa msimu huu.

Carlo Ancelotti ambae hakuwa na furaha hata chembe kufuatia kisago cha mabao matatu kwa moja alichokipokea usiku wa kuamkia hii leo huko kaskazini mwa jiji la London amesema kiujumla kikosi chake kilicheza chini ya kiwango tena kwa kufanya makosa makubwa hivyo endapo kitashindwa kuamka kwa wakati huu bado kuna hasara kubwa inawanyemelea mbele ya safari.

Kwa matokeo ya jana Chelsea wanaendeleza kasumba ya matokeo mabovu toka mwanzoni mwa mwezi uliopita ambapo kuanzia kipindi hicho wameshacheza michezo sita na yote wakiambulia vichapo na endapo watapona basi ni matokeo ya sare.

Kwa upande wa Arsenal wao wamefikisha point 35 ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi ambayo inaongozwa na Man Utd.


No comments:

Post a Comment