Kiungo wa klabu ya Chelsea Frank James Lampard ambae hii leo atakiongoza kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Denmark, amekanusha uvumi unaodai kwamba asilimia kubwa ya wachezaji wa Uingereza wamekua wakionyesha viwango duni kwa makusudi wanapoitwa kwenye timu ya taifa kwa kuhofia huenda wakaumia na kujikuta wakijihatarishia mazingira ya kuvitumikia vilabu vyao ipasavyo.
Frank James Lampard amakanusha uvumi huo baada ya kuulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Copenhagen, ambapo amesema suala hilo halina ukweli wowote na wao kama wachezaji wamekua wakicheza kwa moyo wao wote kwa ajili ya kulitetea taifa lao.
Amesema yeye binafsi hujisikia ufahari pale anapovaa jezi ya timu ya taifa ya Uingereza na kujihisi ni mtu mwenye thamani kubwa ambae anawatetea mashabiki wa taifa lake ambao mara nyingi wamekua wakiwapa ushirikiano kwa kuwafuata popote pale wanapokwenda hapa duniani.
Katika hatua nyingine Lampard ameelezea kufurahishwa na uteuzi wa kuwa nahodha katika kikosi cha Uingereza ambapo kwa mara ya mwisho uteuzi huo ulimuangukia toka kwenye utawala wa Steve McLaren.
Amesema ni faraja kubwa kuwa kiongozi wa timu kama ya Uingereza hivyo atatumia ujuzi na juhudi zake kuwaongoza wachezaji wengine kikosini ili waweze kufanya kweli katika mchezo wa usiku huu.
Lampard pia akazungumzia kutumia uzoefu wa kuongoza akiwa uwanjani ambapo ameahidi kubadilika kutokana na mazingira kwani mara nyingi ameshawahi kuwa nahodha kwenye kikoso cha Chelsea lakini akasisitiza kwamba uongozi wa klabu ni tofauti na uongozi wa timu ya taifa.
Wakati huo huo kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza Fabio Capello amethibitisha kumuanzisha kikosni kiungo wa klabu ya Arsenal Jack Wilshire ambae amedai amefikia kiwango hicho baada ya kumtazama kwa kipindi kirefu kilichopita.
Amesema toka mwanzoni mwa msimu huu kiungo huyo amekua akionyesha uwezo mzuri na amezungumza na meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger ambapo amemuhakikishia kiungo huyo ni mzuri pia kutumika katika nafasi ya ushambuliaji pia.
No comments:
Post a Comment