
FIFA wametoa tamko la kutomruhusu kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina Diego Maradona kuhudhuria hafla ya upangaji wa makundi ya fainali za kombe la dunia siku ya ijumaa huko mjini Cape Town Afrika kusini.
Katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke amesema Maradona, haruhusiswi kufika katika hafla hiyo kufuatia adhabu aliyopewa na shirikisho hilo ya kutojihusishwa na masula ya soka kwa muda wa miezi miwili.
FIFA wametoa taarifa hizo huku kukiwa na fununu zinazoeleza kwamba tayari Maradona yupo mjini Cape Town akisubiri hafla hiyo.
FIFA walilazimika kumpa adhabu hiyo Maradona mnamo November 15 mwaka huu pamoja na kumtoza faini ya paund zaidi ya 14,000, kufuatia kuwatusi waandishi wa habari baada ya mchezo wa kusaka nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia dhidi ya Uruguay ambapo Argentina walishinda bao moja kwa sifuri katika mchezo huo.
Maradona, mwenye umri wa miaka 49, licha ya kuadhibiwa huko, alilazimika kuomba radhi kwa kitendo alichokifanya huku akikielezea kilisababishwa na hasira alizokuwa nazo wakati Argentina ikisaka nafasi ya kuelekea nchini Afrika kusini kucheza fainali za kombe la dunia.
No comments:
Post a Comment