
Beki wa pembeni wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani klabu ya Bayern Munich Philipp Lahm ameteuliwa kuwa nahodha mbadala kwenye timu ya taifa ambayo itashiriki kwenye fainali za kombe la dunia.
Philipp Lahm mwenye umri wa miaka 26 ameteuliwa kuwa nahodha mbadala baada ya nahodha na kiungo wa timu hiyo ya taifa ya ujerumani Michael Ballack kuumia kifundo cha mguu mwanzoni mwa mwezi huu.
Akitangaza maamuzi ya kumpa unahodha beki huyo kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew amesema anaamini Lahm ataweza kufanya maamuzi yaliyo sahihi ya kuwaongoza wenzake watakapokua kwenye fainali za kombe la dunia huko nchini Afrika kusini.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Philip Lahm kuteuliwa kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani aliyoichezea michezo 64 toka alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew amemteua kipa wa klabu ya Schalke O4 Manuel Neuer kipa namba moja wa kikosi chake ambacho kimepangwa kundi la tatu lenye timu za Ghana, Serbia na Australia.
No comments:
Post a Comment