
Uongozi wa klabu ya West Ham Utd hii leo umemtangaza Avram Grant kuwa meneja mpya wa klabu hiyo kwa muda wa miaka minne ijayo.
Grant mwenye umri wa miaka 55, ametangazwa kuwa meneja wa klabu hiyo ya jijini London nchini Uingereza, baada ya kutimuliwa kwa Gianfranco Zola mwishoni mwa msimu wa mwaka 2009-10 kufuatia kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa klabuni hapo.
Sababu kubwa iliyomuondoa Gianfranco Zola ilikuwa ni kushindwa kuiwekea mazingira mazuri ya kiushindani West Ham utd ambayo ilimaliza katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi kuu.
Akizungumza mara baada ya kumtambulisha kwa waandishi wa habari, mmiliki mwenza wa klabu hiyo David Sullivan amesema wanaamini meneja huyo wa kimataifa toka nchini Israeli atafikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake Avram Grant ametanabai kwamba kwake imekua faraja kubwa kuajiriwa kwenye klabu hiyo na ndoto zake za kuingoza West Ham Utd katika hali iliyo salama hii leo zimetimia.
Itakumbukwa kuwa kabla ya Avram Grant hajatambulishwa kuwa meneja wa klabu ya West ham Utd alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya kuinoa klabu ya Portsmouth iliyoshuka daraja kutoka ligi kuu hadi ligi daraja la kwanza nchini Uingereza.
Avram Grant pia atakumbukwa kwa juhudi zake za kuifikisha Chelsea kwenye hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya mwaka 2008, na kwa bahati mbaya hakufikia malengo ya kuwa bingwa wa michuano hiyo baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penati na Man utd.
No comments:
Post a Comment