
Nahodha na beki wa klabu ya Chelsea John Terry anahofiwa huenda ikamchukua muda wa mwezi mmoja kuwa nje ya uwanja kufuatia jeraha la mguu linalomsumbua toka kati kati ya juma lililopita.
Taarifa rasmi toka ndani ya klabu hiyo ya jijini London zimeeleza kuwa beki huyo anahofiwa kuendelea kuwa nje kwa kipindi hicho kufuatia hali yake kwenda tofauti na namna ilivyokua ikifikiriwa huku jopo la madaktari klabuni hapo lilikua likiamini huenda beki huyo angerejea uwanjani mwishoni mwa juma hili.
Taarifa hizo zimeendelea kubainisha kwamba Terry ameshauriwa kuchukua muda mwingine mrefu kupumzika ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida huku aikihofiwa kuwa endapo atarejea mapema huenda akatonesha jeraha linalomkabili kwa sasa.
Hata hivyo taarifa hizo zimeonekana kuwashtua wengi wanaohusika na klabu ya Chelsea ambapo kwa nyakati tofauti hii leo wamekaririwa wakisema tatizo la ulinzi lililojitokeza mwishoni mwa juma lililopita kwenye mchezo dhidi ya Sunderland huenda likaendelea kujitokeza kwa kiasi kikubwa.
Katika hatua nyingine winga wa klabu ya Chelsea Florent Malouda amewataka wanachelsea uliwemnguni kote kutokua na hofu na kikosi chao baada ya matokeo mabovu yaliyopatikana mwishoni mwa juma lililopita.
Winga huyo ambae kwa sasa yupo na kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa ametoa uhakika huo alipozungumza na waandishi wa habari huku akiwataka Wanachelsea kubaini kwamba kikosi chao kina kila sababu ya kutetea ubingwa wao na nafasi waliopo sasa bado ni sehemu ya kuendelea kutamba.
Florent Malouda pia ameshindwa kuzungumzia suala la kuondoka kwa aliekua meneja msaidizi wa kikosi cha klabu ya Chelsea Ray Wilkins ambae anatajwa huenda kukosekana kwa mchango wake ilipelekea hatua ya kufungwa na Sunderland mabao matatu kwa sifuri.
No comments:
Post a Comment