
Jacob 'Ghost' Mulee aliekuja nchini kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya ametangaza kubwaga manyanga baada ya kikosi chake kukubali kisago cha mabao mawili kwa sifuri toka kwa mabingwa watetezi wa michuano ya Tusker Senior challenge Cup timu ya taifa ya Uganda The Cranes.
Mulee ametangaza kuachia nafasi hiyo huku akisema yu tayari kubebeshwa mzigo wa lawama, kufuatia kikosi chake kushindwa kupata point hata moja katika michezo ya hatua ya makundi iliyofikia kikomo jana kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Kocha huyo ambae alikubali kuiongoza timu ya taifa ya Kenya kwa mara ya tatu katika maisha yake ya ufundishaji soka, amevieleza vyombo vya habari hapa nchini kwamba alikuja kwenye michuano ya Tusker Senior challenge Cup na wachezaji wazuri kutoka kwenye ligi ya nchini kwao lakini hakuna mafanikio aliyoyapata hivyo ameona ni bora akae pembeni.
Hata hivyo kufungwa kwa timu ya taifa ya Kenya katika michezo yote ya kundi la tatu, huenda kukawa kumechangiwa na matatizo ya mchezo wa soka yanayoendelea nchini Kenya ambapo kabla ya Harambee Stars haiwasili nchini palitokea tafrani ya vikosi viwili kutajwa.
Mbali na tatizo hilo pia wachezaji wa Harambee Stars waliokuja nchini wamekua wakidai posho zao kutoka kwenye uongozi wa shirikisho la soka nchini Kenya hatua mbayo iliwafanya watishie kutokwenda uwanjani hapo jana.
No comments:
Post a Comment