Aliekua mkuu wa kamati ya maandalizi ya fainali za kombe la dunia kwa mwaka 2010 huko nchini Afrika kusini, Daniel Alexander Jordaan, ametangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho la soka barani Afrika CAF.
Daniel Alexander Jordaan ametangaza maamuzi hayo huku zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa mkutano wa uchaguzi ambao umepangwa kurindima mjini Khartoum nchini Sudan Februari 23.
Sababu kubwa iliyotolewa na Daniel Alexander Jordaan kujiondoa katika kinyang’anyiro ni kutaka kutoa nafasi kwa yeye kujiandaa vyema kwa ajili ya kuwania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho la soka ulimwenguni kote FIFA ambapo pia ameomba nafasi hiyo.
Amesema itakuwa ni vigumu kwake kuzitumikia nafasi za ujumbe wa CAF pamoja na FIFA endapo atapata hivyo ameona ni bora awaachie wagombea wenzake kuwania nafasi ndani ya CAF na yeye kutazama mbele zaidi.
Kujiondoa kwa Jordan sasa kunaufanya ukanda wa kusini mwa bara la Afrika kusaliwa na wagombea wawili wanaowania nafasi ya ujumbe wa CAF ambao ni Kalusha Bwalya toka nchini Zambia pamoja na Suketu Patel kutoka visiwa vya Shelisheli.
No comments:
Post a Comment