Baada ya kufanikiwa kuandaa fainali za mataifa ya bara la Afrika chini ya umri wa miaka 17, ambazo zimefikia tamati mwishoni mwa juma lililopita, serikali ya nchini Rwanda imetangaza kufanya juhudi kwa lengo la kuiwezesha nchi hiyo kuandaa fainali zingine za kimataifa.
Tamko hilo la serikali ya nchini Rwanda limetolewa na waziri wa michezo wa nchini humo Joseph Habineza ambapo amesema haoni sababu ya kushindwa kuwashawishi viongozi wa chama cha soka (FERWAFA) kutuma maombi CAF ya kuandaa fainali nyingine za kimataifa.
Amesema kwa asilimia 100 fainali za mataifa ya bara la afrikla kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zimefanikiwa na hatua hiyo imekua chanzo cha serikali ya raisi Paul Kagame kufikiria ni vipi wataendelea kuandaa fainali nyingine za kimataifa.
Joseph Habineza amebainisha wazi kwamba kwa sasa serikali pamoja na viongozi wa chama cha soka nchini Rwanda wanafikiria kutuma maombi ya kuandaa fainali za mataifa bingwa za bara la Afrika CHAN za mwaka 2016 kisha baada ya hapo watafikiria kutuma maombi ya kuandaa fainali za mataifa ya bara la Afrika miaka ya baadae.
Mbali na serikali ya Rwanda kufurahishwa na utaratibu wa fainali za mataifa za bara la Afrika chini ya umri wa miaka 17, Joseph Habineza pia ameeleza kwamba viongozi wa shirikisho la soka barani Afrika CAF waliokuwepo nchini Rwanda katika kipindi chote za michuano hiyo nao wamefurahishwa na hatua hiyo na kwa kiasi fulani wamekua wakiwashawishi kutuma maombi zaidi ya kuandaa fainali zingine.
No comments:
Post a Comment