KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Monday, July 11, 2011

ARSENE WENGER ATAMBA KUWABAKISHA WACHEZAJI WAKE.



Matumaini ya klabu za mjini Manchester kumsajili kiungo wa kifaransa Samir Nasri yamepigwa kumbo kufuatia meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger kutangaza uwezekano wa mchezaji huyo kubaki kundini.

Arsene Wenger ametoa uhakika huo akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili nchini Malaysia walipokwenda kujiandaa na msimu mpya wa ligi ambao utaanza kutimua vumbi lake kati kati ya mwezi August.

Amesema mchezaji huyo bado ni mwenye furaha ya kuendelea kuitumikia Arsenal na amekua akionyesha dalili zote za kuendelea kubaki klabuni hapo licha ya maneno mengi kuzunguzwa kupitia vyombo vya habari juu ya kutakiwa na klabu za Man Utd pamoja na Man city.

Hata hivyo ameahidi kufanya nae mazungumzo wakiwa nchini Malaysia ambapo siku ya jumatano watacheza mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya kikosi maalum cha wachezaji kumi na moja cha nchi hiyo.

Katika hatua nyingine mzee huyo wa kifaransa amegusia hatua ya kubaki kwa nahodha na kiungo wa kikosi chake Cesc Fabregas ambae amekua akihusishwa na taarifa za kutaka kusajiliwa na klabu iliyomkuza ya FC Barcelona.


Amesema kiungo huyo pia ana imani kwamba atabaki kundini licha ya kuachwa kwenye safari ya nchini Malaysia kufuatia maumivu ya misuli yanayomsumbua kwa kipindi kirefu.

Arsenal Wenger amesafiri na kikosi cha wachezaji 23 ambacho kimemjumuisha kinda wa kijapan Ryo Miyaichi aliejiunga na Arsenal mwezi januari na kupelekwa kwa mkopo nchini Uholanzi kwenye klabu ya Feyenoord, Emmanuel Frimpong aliekua majeruhi msimu uliopita pamoja na beki Carl Jenkinson aliesajiliwa katika kipindi hiki akitokea Charlton Athletics.

Wachezaji walioachwa katika safari hiyo ni Cesc Fabregas ambae ni majeruhi, Manuel Almunia, Emmanuel Eboue pamoja na mshambuliaji Nicklas Bendtner ambao huenda wakauzwa.

Mara baada ya mchezo wa siku ya jumatano utakaochezwa huko mjini Kuala Lumpur kikosi cha Arsenal kitaelekea nchini China kucheza na Hangzhou Greentown siku ya jumamosi.

No comments:

Post a Comment