
Meneja wa klabu ya Liverpool King Kenny Dalglish ameonyesha matumauini ya kumtumia kiungo na nahodha wa klabu hiyo Steven Gerrard pamoja na kipa Pepe Reina katika michezo ya mwanzo wa msimu wa mwaka 2011-12.
King Kenny Dalglish ameonyesha matumaini hayo kwa kusema wachezaji hao waliowaacha nchini Uingereza kwa ajili ya kufanyiwa matibabu pamoja na kufanya mazoezi mepesi, wanaendelea vizuri kufuatai taarifa anazozipokea kutoka kwenye jopo la madaktari.

Akiwa mjini Hangzhou nchini China sanjari na kikosi chake ambacho kitakua nchini humo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi, amesema Steven Gerrard kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita amekua akisumbuliwa na nyonga na wamemuacha nchini Uingereza akiwa katika hali nzuri.
Lakini pamoja na kuonyesha matumaini hayo kwa Gerrard, King Kenny Dalglish akagusia tena hali ya kipa Pepe Reina kwa kusema mwezi uliopita alifanyiwa upasuaji kufuatai matatizo ya ngiri yanayomsumbua na amekua akiendelea vyema.

Katika hatua nyingine King Kenny Dalglish amemtambulisha kiungo mpya wa klabu hiyo Charlie Adam kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hii leo mjini Hangzhou nchini China kwa kusema amefurahishwa na hatua za kukamilika kwa usajili wa mchezaji huyo alieitumikia Blackpool msimu uliopita.
Hata hivyo meneja huyo akashindwa kuzungumzia fununu za usajili wa wachezaji wengine zinazoendelea katika vyombo mbali mbali vya habari mara baada ya kuulizwa swali hilo ambalo lilimlenga winga wa kiingereza Stewart Downing.

Kiungo huyo pia akaanisha wazi kwamba katu hatoidharau Blackpool zaidi ya kuiheshimu na kuithamini lakini kubwa zaidi lililo mbele yake ni kuhakikisha anaitumikia Liverpool kwa moyo wake wote na kufikia malengo yaliyowekwa.
No comments:
Post a Comment