KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Friday, September 30, 2011

SAKATA LA CARLOS TEVEZ LAENDELEA KUSUMBUA UINGEREZA.Meneja wa mabingwa wa soka nchini Uingereza Man Utd Sir Alex Ferguson amemuunga mkono meneja wa klabu pinzani ya Man city Roberto Mancini kufuatia msimamo wake wa kutomuhitaji mshambuliaji kutoka nchini Argentina Carlos Tevez.

Sir Alex Ferguson amesema msimamo wa meneja huyo kutoka nchini Italia unaonyesha ni vipi alivyo na maamuzi yenye nguvu ndani ya klabu ya Man City ambayo ana hakika haimtazami yoyote yule klabuni hapo kwa uwezo ama umaarufu alionao.

Amesema mchezaji siku zote anastahili kutii amri anayoamrishwa na mkuu wake wa kazi na yeye binafsi hakufurahishwa na kitendo alichokionyesha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka, 27 ambae pia aliwahi kuwa chini yake huko Old Trafford.

Na aliekua kiungo wa klabu ya Man Utd, Paul Scholes amesema anamuonea huruma Carlos Tevez kutokana na tukio lililojitokeza katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya FC Bayern Munich uliochezwa usiku wa kuamkia siku ya jumatano.

Paul Scholes amesema anamuelewa vizuri Carlos Tevez na kikubwa alichonacho katika tabia ni kuhitaji kucheza kila mara na linapojitokeza jambo kinyume na hilo hukasirishwa na hatua hiyo.

Amesema yeye binafsi anakumbuka mwaka 2001, aliwahi kugoma kutii amri ya Sir Alex Ferguson ambae alimtaka kuingia uwanjani kama mchezaji wa akiba katika mchezo wa kuwania kombe la ligi na matokeo yake alitupwa benchi katika mchezo dhidi ya Liverpool.

Wakati huo huo mmoja wa viongozi wa klabu ya West Ham Utd iliyomsajili Carlos Tevez mwaka 2006 na kumpelekea nchini Uingereza kwa mara ya kwanza akitokea Sports Corinthians Paulista ya nchini Brazil, amesema yupo tayari kumrejesha mshambuliaji huyo Upton Park kwa mkopo.

Taarifa hiyo imetoka huko jijini London huku viongozi wa Man City wakiendelea kutafakari hatua za kumchukulia mshambuliaji huyo baada ya kumsimamisha kwa majuma mawili na pengine huenda adhabu hiyo ikaongezwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi.

Hata hivyo kuna taarifa kwamba wabeba nyundo hao wa London wapo tayari kumlipa Carols Teves mshahara wa paundi 250,000 kwa juma kwa muda wa miezi mitatu, mshahara ambao anaupata kwa sasa huko Etihad Stadium.

Wakati hayo yakijiri mshambuliaji mwingine wa Manchester City Edin Dzeko amemuomba radhi Roberto Mancini kufuatia kitendo cha utovu wa nidhamu alichokionyesha baada ya kutolewa nje katika mchezo dhidi ya Fc Bayern Munich na nafasi yake kuchukuliwa na Nigel De Jong.

Edin Dzeko amesema hakudhamiria kufanya kitendo cha kutupa, Track Sout bali alifanya hivyo baada ya kushindwa kutimiza malengo ya kuisaidia klabu yake ambayo tayari ilikua nyuma kwa idadi ya mabao mawili kwa sifuri.

No comments:

Post a Comment