Maafisa wa serikali ya nchini Kenya wamevifungia kwa muda usiojulikana viwanja viwili vya michezo mjini Nairobi kufuatia vifo vya mashabiki wa soka wanane vilivyotokea mwishoni mwa juma lililopita.
Kufungiwa kwa viwanja hivyo ambavyo ni Nyayo pamoaja na Moi Kassarani kunatoa nafasi kwa jeshi la Polisi nchini Kenya kuanza kufanya uchunguzi wa kubaini nini kilichopelekea vifo vya watu hao waliokua katika harakati za kuutazama mchezo uliowakutanisha mahasimu wakubwa nchini humo Gor Mahia FC dhidi ya AFC Leopards.
Imeelezwa kuwa licha ya vifo hivyo kutokea bado uwanja wa Nyayo ulikua haijafurika mashabiki, huku taarifa nyingine zikieleza kwamba watu hao waliofikwa na umauti walikua katika harakati za kutaka kuingia uwanjani hapo bila kulipa viingilio.
Tayari waziri mkuu wa nchini Kenya Raila Odinga ameshatoa kauli ya kuonyesha matumaini kwamba uchunguzi huo unaoendelea hivi sasa majibu yake yatatolewa mwishoni mwa juma hili na kufahamika nini chanzo cha vifo hivyo kutokea.
Wakati huo huo uongozi wa shirikisho la soka duniani FIFA umeonyesha kusikitishwa na tukio hilo na tayari raisi wa shirikisho hilo Sepp Blatter ametuma salamu za rambirambi kwa wapenzi wa soka wa Kenya.
No comments:
Post a Comment