Baada ya kumtimua kazi Sam Allardyce, wamilikiwa wa klabu ya Blackburn Rovers wamethibitisha kufanya mawasiliano na aliekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina Diego Armando Maradona.
Wamiliki wa klabu hiyo ambao ni ndugu wawili kutoka nchini India Balaji Rao pamoja na Venkatesh Rao, wamethibitisha taarifa za kuwepo kwa mawasiliano hayo lakini wametoa msimamo wa kuendelea kumtumia meneja msaidizi Steve Kean kushika pahala pa Sam Allardyce mpaka mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa iliyotolewa kupitia kwa mwenyekiti wa klabu ya Blackburn Rovers mwana mama Anuradha Desai imeonyesha kwamba licha ya kuwepo kwa mawasiliano hayo bado haijajulikana nini hatma ya kuajiriwa kwa Diego Armando Maradona huko Ewood Park kufuatia mikakati rasmi kutokuwekwa wazi.
Hata hivyo mwana mama huyo amesema bado wana imani meneja msaizi Steve Kean ana uwezo wa kutosha wa kutimiza mikakati iliyowekwa klabuni hapo mpaka mwishoni mwa msimu huu ambapo wana aamini mikakati ya kumtangaza meneja mpya itakua imeiva.
Wakati huo huo nahodha msaidizi wa Rovers Ryan William Nelsen amezungumzia masikitiko yake ya kutimuliwa kwa aliekua meneja wao Sam Allardyce ambapo amedai kwamba hakuamini maamuzi yaliyochukuliwa na viongozi wa juu klabuni hapo ya kumfukuza Big Sam.
Amesema Big sam aliishi nao vizuri na alijitahidi kadri ya uwezo wake kuhakikisha wanafanya vyema katika michezo yao ya ligi ya ile ya michuano mingine wanayoshiriki msimu huu na anaamini meneja huyo angefikia mikakati iliyowekwa klabuni hapo.
Uchungu wa kutimuliwa kwa Sam Allardyce pia umemgusa mwenyekiti wa chama cha mameneja wa vilabu vya soka nchini Uingereza Howard Wilkinson ambapo amesema Big Sam bado alikua na sifa thabiti za kuendelea kukinoa kikosi cha Rovers kufuatia umakini wa kazi zake anazozifanya.
Amesema mpaka sasa bado haelewi nini kilichopelekea kutimuliwa kwake huko Ewood Park il-hali kikosi cha Rovers kikiwa kinashikilia nafasi ya kumi kwenye msimamo wa ligi.
No comments:
Post a Comment