KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Saturday, December 25, 2010

Leonardo Nascimento de Araújo NDIE MRITHI WA BENITEZ.


Siku mbili baada ya uongozi wa klabu bingwa duniani Inter Milan ya nchini Italia kuthibitisha umemtimua kazi Rafael Benitez, usiku wa kuamkia hii leo uongozi huo ulimtangaza Leonardo Nascimento de Araújo kuwa meneja wa klabu hiyo.

Leonardo Nascimento de Araújo amekubalia kukichukua kikosi cha mabingwa hao wa nchini Italia kwa mkataba maalum ambao utamuwezesha kuwepo huko Stadio Giuseppe Meazza hadi mwishoni mwa msimu huu.

Meneja huyo toka nchini Brazil ambae msimu uliopita alikinoa kikosi cha AC Milan amepewa jukumu hilo huku uongozi wa klabu ya Inter Milan ukiamini anaweza kurejesha hadhi ndani ya kikosi chao ambacho kimekua hakifanya vizuri katika michezo ya ligi ya nyumbani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao wa klabu ya Inter Milan zimeeleza kwamba Leonardo ana vigezo vya kutosha ambavyo vinakidhi haja ya kukinoa kikosi cha klabu hio hivyo uongozi hauna shaka nae na ndio maana umekubali kuingia nae mkataba wa muda mfupi kwa minajili ya kuokoa jahazi.

Benitez ameondoka klabuni hapo ikiwa ni siku chache tu baada ya kuiwezesha Inter Milan kutwaa ubingwa wa dunia mbele ya mabingwa wa barani Afrika TP Mazembe ambao walikubalia kisago cha mabao matatu kwa sifuri.

Kama itakumbukwa vyema Benitez alipewa jukumu la kukinoa kikosi cha Inter Milan baada ya kutimuliwa na uongozi wa klabu ay Liverpool ambao haukuridhishwa na kazi yake aliyoifanya msimu uliopita ambayo ilikifanya kikosi cha The Reds kumaliza nje ya mpaka wa timu nne bora katika msimamo wa ligi kuu ya nchini Uingereza.

Kuelekea kwake Inter Milan kulipewa nafasi kubwa kufuatia kuondoka kwa aliekua meneja wa klabu hiyo Jose Mourinho ambae alitimkia Real Madrid baada ya kuiwezesha The Nerazzurri kutwaa ubingwa wa vikombe vitatu ambavyo ni kombe la nchini Italia, kombe la ubingwa wa ligi ya nchini Italia sambamba na ligi ya mabingwa barani ulaya.

No comments:

Post a Comment