Meneja wa klabu ya Man City Roberto Mancini amesema baada ya ushindi wa jana wa mabao matatu kwa moja walioupata mbele ya Newcastle Utd, sasa kilichosalia kwa kikosi chake ni kurejesha heshima ya kushinda kila wanapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani City Of Manchester.
Mancini ambae alionekana mwenye furaha mara baada ya kipyenga kupulizwa katika mchezo wa jana uliopigwa huko St James Park amesema ushindi huo umewapa hamasa ya kuanza mikakati hiyo mara baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Everton ambao waliwanyuka mabao mawili kwa moja wakiwa nyumbani.
Amesema mchezo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa sana kwao lakini alikubaliana na kile kilichotokea, ila akaendeleza msisitizo wa kuhakikisha kasumba ya kupoteza michezo ya nyumbani inafutika kwenye vichwa vywa wachezaji wake.
Hata hivyo Mancini ameeleza kwamba mchezo wa jana dhidi ya Newcastle Utd haukuwa rahisi kama wengi wanavyofikiri kufuatia kupata mabao mawili ya haraka katika dakika za mwanzoni.
Nae meneja wa klabu ya Newcastle Utd Alan Pardew ameonyesha kujifariji baada ya kuchapo cha mabao matatu kwa moja mbele ya Man City ambapo amesema pamoja na kupokea kibano hicho bado wachezaji wake walionyesha kandanda safi wakati wote licha ya kuwepo kwa makosa kwenye idara ya ulinzi.
Amesema hakuna kibaya kilichoonekana kwa wachezaji wake ambao walionyesha namna gani walivyokua na hamu ya kutaka kusawazisha baada ya kupatikana kwa bao la kwanza lililofungwa na Andy Callor lakini amekiri wachezaji wake pamoja na yeye binafsi walikatishwa tamaa baada ya wapinzani wao kupachika bao la tatu kupitia kwa Carlos Teves.
Wakati huo huo beki wa kimataifa toka nchini Uingereza na Newcastle Utd Steven Taylor, amefanikisha malengo ya uongozi wa klabu hiyo baada ya kukubali kusaini mkataba mpya.
Steven Taylor amekamilisha malengo hayo baada ya kuwaweka kwenye wakati mgumu viongozi wa klabu hiyo ya St James Park kutokana na fununu ambazo zilieleza kwamba beki huyo ana asilimia chache za kuendelea kuichezea The Magpies msimu ujao.
Steven Taylor amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano ambao sasa utamuweka huko St James Park hadi mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment