Beki wa kushoto wa klabu ya Chelsea Ashley Cole amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa nchini Uingereza kwa mwaka 2010.
Ashley Cole amechaguliwa katika nafasi hiyo na mashabiki wa soka nchini Uingereza ambao walipata nafasi ya kupiga kura zao kupitia mtandao wa chama cha soka nchini humo huku nahodha na kiungo wa klabu ya Liverpool Steven George Gerrard akishika nafasi ya pili na nafasi ya tatu imechukuliwa na winga wa klabu ya Manchester City Adam Johnson.
Mashabiki wa soka nchini humo walipata nafasi ya kupiga kura za kuwachagua wachezaji hao kwa kipindi cha mwaka mzima huku wachezaji 44 waliopata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kwa mwaka 2010 wakishirikishwa katika utaratibu huo.
Sababu kubwa iliyompa nafasi kubwa Ashely Cole kuibuka na ushindi huo ni kufanikiwa kucheza vyema katika michezo ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Misri, Mexico pamoja na Ufaransa ambapo kwa upande wa wapinzani wake hawakufanikiwa kucheza sehemu ya michezo hiyo.
Tuzo hiyo ya uchezaji bora wa nchini Uingereza kwa mwaka 2009 na 2008 ilichukuliwa na mshambuliaji wa klabu ya Man utd Wayne Rooney, mwaka 2007 ilichukuliwa na Steven George Gerrard, mwaka 2006 ilikwenda kwa Owen Hargreaves, mwaka 2005 na 2004 ilichukuliwa na Frank Lampard huku David Beckham akiwa wa kwanza kutwaa tuzo hiyo mwaka 2003.
No comments:
Post a Comment