Beki wa kimataifa toka nchini Brazil na klabu ya Fc Barcelona Daniel Alves da Silva amesema suala la kukomesha vitendo vya ubaguzi wa rangi nchini Hispania haliwezi kukoma kama wengi wanavyotarajia.
Daniel Alves da Silva imemlazimu kulisema hilo baada ya kukiri kuchoshwa na vitendo vya ubaguzi wa rangi anapokua uwanjani akiitumikia klabu yake katika michezo ya michuano mbali mbali.
Amesema mbali na yeye binafsi kukutana na tatizo hilo pia familia yake imekua ikikumbana na vitendo hivyo, hatua ambayo inamuumiza yeye binafsi, lakini amebainisha wazi kwamba hana budi kuizoea hali hiyo kutokana na mazingira ya watu anaoishi nao.
Amesema mashabiki wamekua wakimuita nyani anapokua ndani na nje ya uwanja lakini hujitahidi kukabiliana na hali ya hasira na mwisho wa siku anafanikiwa katika hilo na kujifariji kwa kujiliwaza mawazoni kwa kutambua kwamba huenda wanaombagua kwa rangi yake hawana elimu ya kutosha.
Vitendo vya ubaguzi wa rangi nchini Hispania tayari vilishawahi kulalamikiwa na mshambuliaji wa klabu ya Inter Milan ya nchini Italia Samuel Eto’o wakati akiitumikia klabu ya Barcelona, mshambuliaji wa sasa wa klabu ya Sevilla Frédéric Oumar Kanouté pamoja na wachezaji wengine wenye asili ya bara la Afrika, lakini bado linaonekana kuendelea kushamiri.
No comments:
Post a Comment