Meneja wa klabu ya Barcelona Josep "Pep" Guardiola i Sala amekubalia kusaini mkataba mpya na klabu hiyo ambao utamuweka huko Camp Nou hadi mwishoni mwa msimu ujao.
Josep "Pep" Guardiola i Sala amekubalia kusaini mkataba huo, huku mkataba wake wa sasa ukitarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu na kulikua na dalili zote kwa meneja huyo kuachia ngazi na kumpisha mwingine aendelee na shughuli ya kusaka mataji klabuni hapo.
Tayari uongozi wa klabu ya Barcelona umeshathibitisha kwamba Guardiola atasaini mkataba mpya ndani ya siku kadhaa zijazo na matarajio yao ni kutaka kuona mazuri yaliopo sasa yanaendelezwa na meneja huyo aliemrithi Franklin Edmundo Rijkaard mwaka 2009.
Josep "Pep" Guardiola i Sala mwenye umri wa miaka 40 toka alipoanza kibarua cha kukinoa kikosi cha klabu ya Barcelona, amekua na mafanikio makubwa kufuatia kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, ubingwa wa klabu bingwa duniani, ubingwa wa ligi nchini Hispania pamoja na kombe la mfalme.
Na kwa hivi sasa meneja huyo tayari ameshaanza kuonyesha dalili zote za kutetea taji la ligi kuu ya soka nchini Hispania kufuatia kikosi chake kuongoza ligi kwa tofauti ya point saba dhidi ya mahasimu wao wakubwa Real Madrid.
No comments:
Post a Comment