Uongozi wa chama cha soka nchini Uingereza FA umesema hautimuadhibu nahodha na kiungo wa klabu ya Arsenal Francesc "Cesc" Fàbregas Soler baada ya kudaiwa alimtusi muamuzi Lee Mason aliechezesha mchezo wa kuamkia jana dhidi ya Everton huko Emirates Stadium.
Madai ya Cesc Fabregas kumtukana muamuzi yalitolewa na meneja wa klabu ya Everton David William Moyes mara baada ya mchezo huo ulioshuhudia Arsenal wakiibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja, ambapo alisema nahodha huyo wa The Gunners alimtolea maneno makali Lee Mason wakati wa mapumziko.
Katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia hii leo na chama cha soka nchini Uingereza imeeleza kwamba hakuna uthibitisho wowote ambao unaweza kumtia hatiani kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23.
FA imeeleza kwamba endapo kwenye taarifa za muamuzi suala hilo lingeorodheshwa kulikua na sababu kubwa ya kesi hiyo kujadiliwa lakini hakuna mahala popote panapothibitisha Cesc Fabregas alimtusi muamuzi.
Cesc Fabregas anadaiwa kufanya hivyo baada ya kukasirishwa na maamuzi ya Lee Mason ya kuruhusu bao la mshambuliaji wa klabu ya Everton Luois Laurent Saha ambae alikua ameotea kabla ya kupokea pasi iliyokuwa imeguswa na beki wa klabu ya Arsenal.
No comments:
Post a Comment