Siku moja baada ya ushindi mnono wa mabao manne kwa moja uliopatikana chini ya kocha mpya wa timu ya taifa ya Ghana Goran Stevanovic dhidi ya timu ya taifa ya Togo, mashabiki wa soka nchini Ghana wametoa pongezi kwa kocha huyo wa kimataifa toka nchini Serbia.
Mashabiki hao wametoa pongezi hizo kupitia vyombo mbali mbali vya habari nchini Ghana ambapo wamesema wameridhishwa na uwezo mkubwa ulioonyeshwa na timu yao ya taifa iliyokua ugenini huko nchini Ubelgiji ikicheza mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Togo.
Mashabiki hao wamesema safu ya ushambuliaji ya kikosi chao katika mchezo huo ilionekana kuwa na makali ya ajabu mbali na ilivyokua kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka 2010, hatua ambayo wameipokea kwa mikoni miwili na kuamini safari ya kuelekea nchini Equatorial Guinea pamoja na Benin kushiriki fainali za mataifa ya bara la Afrika ipo kama kawaida endapo wataendelea kucheza kama walivyocheza jana.
Hata hivyo baadhi ya mashabiki nchini Ghana wamesema hawakubahatika kuuona mchezo huo kutokana na televisheni za kijamii kushindwa kuonyesha mpambano huo, lakini wamepokea taarifa kutoka kwa mashabiki walioushuhudia mchezo huo na wameonyesha kuridhishwa na kile kinachosemwa.
Baada ya mchezo wa jana kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ghana Goran Stevanovic atarejea tena kibaruani March 25, kwa lengo la kukiwezesha kikosi chake kusaka ushindi dhidi ya Congo Brazzaville katika mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment