Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Afrika kusini Bafana Bafana Pitso John Mosimane ametangaza kuwaacha wachezaji wa klabu ya Mamelodi Sundown kwenye kikosi chake ambacho kwa sasa kinajiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars.
Wachezaji hao walioachwa kwenye kikosi cha Bafana Bafana ni Katlego Mphela pamoja na Teko Tsholofelo Modise ambao wamedaiwa kutokua na nidhamu.
Pitso John Mosimane amesema wachezaji hao nidhamu yao imeshuka na hatua hiyo imeonekana kufuatia Katlego Mphela kumshawishi Teko Tsholofelo Modise kuomba uhamisho kwa viongozi wa klabu yake ya zamani ya Orlando Pirates ili aweze kujiunga nae huko Mamelodi Sundowns ambapo hatua hiyo ilifanikiwa.
Amesema lengo kubwa la kuwaacha wachezaji hao ni kutaka kuonyesha ni vipi nidhamu inatakiwa kuzingatiwa kutoka kwenye vilabu vya soka nchini humo ili kesho na kesho kutwa wachezaji wengine wasije wakaiga tabia hiyo chafu ya kushawishiana.
Katika hatua nyingine Pitso John Mosimane amethibitisha kumrejeshea unahodha beki wa klabu ya Portsmouth Teboho Aaron Mokoena ambae alikuwa benchi katika mchezo wa kimataifa wa kirafaiki uliopita dhidi ya timu ya taifa ya Marekani.
Wachezaji wengine walioitwa kikosini ni wa klabu ya Tottenham Hotspurs ya nchini Uingereza Bongani Sandile Khumalo, Steven Jerome Pienaar pamoja na Davide Somma, anaeitumikia klabu ya Leeds Utd.
No comments:
Post a Comment