Hatimae uongozi wa klabu ya West Bromwich Albion umemtimua kazi meneja wa klabu hiyo Roberto Di Matteo.
Uongozi wa klabu ya West Bromwich Albion umefikia maamuzi hayo baada ya kikao cha bodi kukubaliana juu ya kutimuliwa kazi kwa meneja huyo wa kimataifa toka nchini Italia ambae jana alipokea taarifa za kupumzishwa kazi kwa muda.
Sababu kubwa iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo juu ya kufutwa kazi kwa Roberto Di Matteo ni kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa klabuni hapo hatua ambayo inakipeleka pabaya kikosi katika msimamo wa ligi.
Taarifa hizo imeendelea kusisitiza kwamba Roberto Di Matteo ameshindwa kupata uwiyano mzuri wa ushindi katika michezo kadhaa ambapo mpaka hivi sasa kikosi chake kimeshapoteza michezo 13 ndani ya michezo 18 iliyopita ya michuano yote.
Saa chache baada ya kupokea taarifa za kutimuliwa kazi Roberto Di Matteo alituma barua pepe katika vyombo vyote vya habari nchini Uingereza na kueleza masilikito yake kufuatia hatua hiyo.
Roberto Di Matteo amesema alishangazwa na maamuzi ya uongozi wa ngazi za juu ya kumtimua kazi kwa kisingizio cha kufanya vibaya katika michezo ya ligi kuu pamoja na michezo ya michuano mingine hali ambayo ameipinga vikali.
Amesema kimtazamo hajafanya vibaya mpaka sasa hasa ikizingatiwa kwamba yeye ndie aliefanya kila jitihada za kuirejesha klabu hiyo kwenye ligi kuu baada ya kushika nafasi ya pili kwenye ligi daraja la kwanza msimu uliopita.
Amesema mwanzoni mwa msimu huu wakati anaanza pirika pirika za michezo ya ligi hiyo, kikosi chake kilijitahidi kuvishinda vigogo katika viwanja vya nyumbani kwao na sasa ilikua imesalia shughuli ya kucheza nyumbani ambapo kwake ilikua ni rahisi mno kuzipata point tatu muhimu.
Hata hivyo Roberto Di Matteo mwenye umri wa miaka 40 amewatakia kila la kheri wachezaji wa klabu hiyo katika harakati za kupigana hadi mwishoni mwa msimu huu ambapo itawalazimu kujihakikishia nafasi ya kuendelea kuwepo katika kindumbwe ndumbwe cha ligi kuu msimu ujao.
Roberto Di Matteo pia ametoa shukurani kwa viongozi pamoja na mashabiki wa klabu ya West Bromwich Albion kwa ushirikiano waliomuonyesha toka alipokubalia kukinoa kikosi chao mwaka 2009.
Kuondoka kwa meneja huyo wa kimataifa toka nchini Italia, pia kumetoa nafasi kwa msaidizi wake Eddie Newton pamoja na mkurugenzi wa michezo Ade Mafe kuondoka klabuni hapo huku kocha wa kikosi cha kwanza Michael Appleton akipewa jukumu la kukiongoza kikosi cha West Bromwich Albion kwa muda.
Wakati Roberto Di Matteo akisikitishwa na kitendo cha kutimuliwa kazi, aliekua meneja wa klabu ya Liverpool Roy Hodgson ndie anaetajwa sana huenda akapewa kibarua huko The Hawthorns.
Magazeti mbali mbali ya nchini Uingereza yameripoti kwamba meneja huyo anafikiriwa kupewa jukumu la kushika pahala pa Roberto Di Matteo.
No comments:
Post a Comment