
Wafanyakazi wa ujenzi wa viwanja vya soka vya nchini Afrika kusini ambavyo vitachezewa fainali za kombe mwaka 2010 wapo kwenye mlolongo wa makubaliano yatakayowawezesha kupata nyongeza ya mshahara kwa lengo la kumaliza mgomo ulidumu kwa muda wa juma moja.
Wafanyakazi hao ambao idadi yao ni elfu 70 wanaendelea na mlolongo huo huku taarifa zikieleza kuwa baadhi yao wameshaanza kufanya kazi hii leo.
Hapo jana, vyama vya Wafanyakazi na waajiri nchini Afrika kusini walikuwa wakikamilisha majadiliano ya kusaini makubaliano ya mikataba ambayo itawawezesha wafanyakazi wa ujenzi wa viwanja hivyo kulipwa asilimia ya mshahara waliyokuwa wanaihitaji.
Makubaliano yaliyopangwa kuhusiana na nyongeza hiyo bado hayajatangazwa rasmi, lakini inaaminika kuwa waajiri na wafanyakazi wamekubaliana nyongeza ya asilimia 12, ambapo awali wafanyakazi hao walikuwa wakitaka asilimia 13.
Wafanyakazi hao walianza mgomo July 8 mwaka huu kwa madai ya kutaka kuongezewa asilimia ya mshahara wao.
Mgomo huo ulisababisha wasiwasi kwa baadhi ya miji kutoweza kukamilisha muda uliowekwa na kukabidhi viwanja hivyo mwezi Desemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment