
Kipa namba moja wa kikosi cha klabu ya Arsenal Manuel Almunia amesema anaamini kikosi chao msimu ujao kitacheza kwa mtazamo mpya mbali na ilivyokuwa msimu uliopita.
Kipa huyo wa kimataifa toka nchini Hispania amesema wazo hilo linamuijia katika fikra zake kufuatia muonekano wa kikosi chao ambacho kimeongezewa nguvu na wachezaji waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu ambao sasa wanaonekana kuwa fit na kucheza katika viwango vyao vya kawaida.
Almunia mwenye umri wa miaka 32 amewataja wachezaji hao kuwa ni Tomas Rosicky Eduardo huku akimtaja Andrey Arshavin kuwa ni mchezaji ambae hakuweza kuonyesha makali yake kufuatia ugeni aliokuwa nao wakati akisajiliwa klabu hapo mwezi januari mwaka huu.
Hata hivyo Almunia ameongeza kuwa mbali wachezaji hao wenye uzoefu, pia anaamini vijana chipukizi walipo kwenye kikosi chao, nao watakuwa wamejifunza mengi hali ambayo imeleta changamoto katika vichwa vyao na kuwajengea hatua ya kiushindani wanapokuwa mashindanoni.
Amesema katika mchezo wao wa kujipima ubavu uliounguruma mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya klabu ya Barnet na kumalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili, wachezaji wa Arsenal walionyesha umahiri mkubwa na kucheza soka lenye tofauti hivyo hatua hiyo ni moja ya kuona ni vipi walivyobadilika.

Wakati huo huo meneja wa klabu ya Arsenal Arsène Wenger ameutangazia umma wa mashabiki wa klabu hiyo kwamba bado jicho lake laendelea kumuangaza mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Morocco na klabu ya Bordeaux ya nchini Ufaransa Marouane Chamakh.
Arsen Wenger ametangaza hatua hiyo hii leo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ambapo amebainisha wazi kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ndio chaguo lake la kwanza endapo atahitaji kufanya usajili katika kipindi hiki.
Amesema mshambuliaji huyo ana uwezo mkubwa wa kuziba mwanya ulioachwa wazi na mshambuliaji Emmanuel Adebayor ambae siku mbili zilizopita alikamilisha dili la kujiunga na klabu ya Manchester City.

Akionyesha ni vipi alivyo na hamu ya kuongeza mchezaji kwa sasa, wenger amesema ameona mapungufu katika safu ya ushambuliaji wakati kikosi chake kikicheza na klabu ya Barnet mwishoni mwa juma lililopita hivyo upo umuhimu mkubwa wa kufanya hima ya kusajili mshambuliaji ambae anaeweza kuziba nafasi hiyo.
Kauli hiyo ya Arsene Wenger inadhihirishayupo katika harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji mwingine katika klabu hiyo na kuvunja kauli ambayo aliitoa mwishoni mwa juma lililopita katika vyombo vya habari kwa kusema kwamba haoni sababu ya kusajili mshambuliaji kwa wakati huu kutokana na kuwepo kwa jibu hilo ndani ya wachezaji waliosalia klabuni hapo.
No comments:
Post a Comment