
Shirikisho la soka duniani kote FIFA limemtaka aliekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon Arie Haan kulilipa shirikisho la soka la nchi hiyo (Fecafoot) zaidi ya dola za kimarekani 650,000.
FIFA wamemtaka Arie Haan kufanya hivyo baada ya kuabaini alivunja mkataba na shirikisho la soka nchini Cameroon ambao ulikua ukimtaka kukinoa kikosi cha nchi hiyo kwa muda wa miaka miwili toka mwaka 2006-08.
Haan raia wa nchini Uholanzi alikwenda kinyume na mkataba wake baada ya kuondoka nchini Cameroon mwezi Februari mwaka 2007 huku akitoa visingizio vya kuchukizwa na hatua ya maamuzi yake kuingiliwa na viongozi wa (Fecafoot).
Hata hivyo FIFA bado wametoa nafasi kwa kocha huyo kukata rufaa kwa maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yake endapo ataona ameonewa.
Kwa sasa Arie Haan ambae alikua miongoni mwa wachezaji walioifikisha timu ya taifa ya Uholanzi katika hatua ya fainali ya michuano ya kombe la dunia mwaka 1974 pamoja na 1978, anakinoa kikosi cha timu ya taifa ya China na kabla ya hapo alikua akikinoa kikosi Albania.
No comments:
Post a Comment