
Beki wa pembani wa klabu ya Arsenal Bacary Sagna ametangaza vita na aliekua nahodha na beki wa klabu hiyo William Gallas ambae kwa sasa anaitumikia Tottenham Hotspurs.
Bacary Sagna ametangaza vita hiyo huku klabu hizo mbili zikitarajia kuonyeshana kazi katika mchezo wa kesho ambao utaunguruma huko Emirates.
Vita iliyotangazwa na beki huyo mwenye umri wa miaka 27 ni kuhakikisha Gallas anathibitishiwa uwezo wa Arsenal ambayo aliiponda alipokua akijiunga na klabu ya Spurs mwanzoni mwa msimu huu kwa kusema klabu hiyo si lolote si chochote kutokana na kuendelea kufuga vijana kila kukicha.
Hata hivyo Bacary Sagna amesema Gallas ni rafiki yake wa karibu lakini linapokuja suala la mchezo kama wa kesho urafiki unalazimika kuwekwa pembeni na kuuthibitishia ulimwengu kwamba Arsenal ni bora ya klabu ambayo amejiunga nayo kwa majigambo ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wowote msimu huu.
Katika hatua nyingine kiungo wa klabu ya Arsenal Jack Wilshere yu mashakani kucheza mchezo wa kesho dhidi ya Spurs kufuatia maumivu ya mgongo yanayoendelea kumsumbua.
Jack Wilshere hii leo anatarajia kufanyiwa vipimo vya mara ya mwisho ambavyo vitatoa majibu ambayo huenda yakatoa mustakabali wa kucheza ama kutokucheza katika mchezo huo wa kesho ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa klabu hizo mbili.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 18 alilazimika kuondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza iliyopoteza mbele ya Ufaransa kwa kufungwa mabao mawili kwa moja usiku wa kuamkia jana kufuatia matatizo ya mgongo.
No comments:
Post a Comment