
Winga wa kimataifa toka nchini Ufaransa Robert Pires amekamilisha taratibu zote za kuitumikia klabu ya Aston Villa inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Uingereza.
Winga huyo amekamilisha taratibu hizo baada ya kusaini mkataba wa miezi sita klabuni hapo jana na siku ya jumapili anatarajiwa kujumuishwa katika kikosi kitakachoikabili Blackburn Rovers huko Ewood Park.
Robert Pires amesajiliwa huko Villa Park akiwa kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na klabu ya Villareal ya nchini Hispania kumalizika hatua ambayo ilimfanya arejee nchini Uingereza na kufanya mazoezi na kikosi cha klabu ya Arsenal kwa muda wa miezi miwili na kisha alimvutia meneja wa Aston Villa Gerard Houllier ambae amepanga kufanya vyema katika msimu huu wa ligi.
Pires, mwenye umri wa miaka 37, anarejea katika ligi kuu ya soka nchini Uingereza huku mashabiki wengi wakiukumbuka mchango wake alioutoa akiwa na klabu ya Arsenal kuanzia mwaka 2000–2006 ambapo alifanikiwa kuifungia klabu hiyo mabao 84 katika michezo 283 aliyocheza.
Mbali na kukumbukwa kwa mchango alioutoa akiwa na klabu ya Arsenal, winga huyo bado ataendelea kukumbukwa kupitia michezo ya timu ya taifa lake la Ufaransa ambapo alifanikiwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha nchi hiyo kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 1998.
Akiwa na klabu ya Villareal toka mwaka 2006–2010 winga huyo alifanikiwa kucheza michezo 102 na kufunga mabao 13.
No comments:
Post a Comment