
Baada ya kuthibitisha yu tayari kumsajili winga wa kimataifa toka nchini Ufaransa Robert Pires, Meneja wa klabu ya Aston Villa Gerard Houllier bado anaendelea na mipango ya kutaka kukiimarisha zaidi kikosi chake kupitia dirisgha dogo la usajili litakalofunguliwa mapema mwezi Januari mwaka 2011.
Gerard Houllier anaendelea na mipango hiyo huku macho yake akiyaelekeza kwa mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Ufaransa na klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania Karim Benzema ambae kwa sasa ana wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Jose Mourinho.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari meneja huyo wa kifaransa amesema kwa sasa uongozi wa klabu ya Aston Villa unatazama uwezekano wa kuhakikisha wanamshajili Benzema kwa namna yoyote ile.
Amesema utaratibu wa kusajili kwa mshambuliaji huyo ni sehemu ya mipango yake aliyoiwasilisha kwa uongozi wa ngazi za juu klabuni hapo na sasa anafurahishwa na taratubu zinazochukuliwa kwa malengo ya kumkamilishia kazi yake ambayo anaamini mwishoni mwa msimu huu itakuwa nzuri.
Hata hivyo Gerard Houllier amebainisha wazi kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 huenda akawagharimu kiasi kikubwa cha fedha katika utaratibu wa uhamisho wake, kutokana na uongozi wa klabu ya Real Madrid kutaka kurejesha fedha walizozitumia wakati wakimsajili akitokea Olympic Lyon ya nchini Ufaransa, mwaka 2009.
Katika hatua nyingine Gerard Houllier amekanusha taarifa za yeye kuwa kwenye mipango ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Uingereza na klabu ya Man utd Michael Owen, baada ya vyombo vya habari kutangaza hivyo toka jana.
Itakumbukwa kuwa Michael Owen alicheza chini ya uangalizi wa Gerard Houllier alipokua akikiongoza kikosi cha klabu ya Liverpool kama meneja kabla ya kuondoka kwake mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment