
Mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Cameroon pamoja na klabu bingwa barani Ulaya Inter Milan Samuel Eto'o ameomba radhi kwa kitendo cha kumpiga kichwa beki wa klabu ya Chievo Verona pale klabu hizo zilipokutana mwishoni mwa juma lililopita.
Eto'o ameomba radhi huku ikiwa tayari ameshaadhibiwa na chama cha soka nchini Italia baada ya kitendo hicho kuchunguzwa kupitia picha za televisheni ambapo alibaionika kumpiga kwa makusudi beki wa Chievo Verona Bostjan Cesar kichwa cha kifuani.
Radhi zake amezielekeza kwanza kwa meneja wa klabu yake Rafael Benitez ambapo amemtaka amsamehe kwa kosa hilo alilolifanya, pia akawataka radhi wachezaji wenzake wa klabu ya Inter Milan na kisha akamuomba radhi Bostjan Cesar aliemfanyia kitendo hicho.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 pia akaomba radhi kwa mashabiki wake ulimwengu mzima ambapo amewataka waelewe hakufanya kitendo hicho kwa makusudi bali alijikutaka akifanya hivyo kufuatia hasira ambazo zilisababishwa na Bostjan Cesar kumpiga ngumi ya shingoni alipokua katika jukumu la kumkaba.
Licha ya kuadhibiwa kwa kutokucheza michezo mitatu ya ligi kuu ya soka nchini Italia, pia Samuel Eto’o ametozwa faini ya Euro Elfu 30 ambazo ni sawa na Paund za Uingereza 25,600.
No comments:
Post a Comment