
Meneja wa klabu bingwa nchini Uingereza Carlo Ancelotti amesema anaamini kikosi chake kitaonyesha mustaklabali wa msimu huu mwishoni mwa juma hili pale kitakaposhuka dimbani kucheza na Tottenham Hotspurs.
Carlo Ancelotti ambae amekishuhudia kikosi chake kikipata matokeo mabovu kwa muda wa majuma manne mfululizo amesema mchezo huo anatambua utakua mgumu lakini ukweli ni kwamba mchezo huo ndio utatoa taswira ya nini walichokiandaa kwa msimu huu.
Alipoulizwa ni kwa nini anaonyesha wasi wasi juu ya Spurs na kuuchukulia mchezo dhidi yao ndio kipimo meneja huyo wa kimataifa toka nchini Italia akabainisha wazi kwamba kikosi cha Spurs ni kizuri na anaamini ndicho kitakua kipimo kizuri kwao.
Mbali na kuonyesha hofu hiyo, bado Anceloti ameendelea kuwa na msimamo wake wa kusema kikosi chake ni kizuri na kimekua kikionyesha uwezo wa kijiamini kinapokua uwanjani licha ya matokeo mabovu kuwaandama.
Chelsea ambao walifanikiwa kuongoza ligi kwa kipindi cha miezi minne mfululizo, kwa sasa wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na point 30 baada ya matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Everton yaliyopatikana mwishoni mwa juma lililopita.
Hata hivyo yasemekana ndani ya klabu hiyo ya jijini London kuna jambo linaendelea ambalo sio zuri na pengine limekua likichangia matokeo mabovu yanayopatikana.
Mmoja wa waandishi wa habari nchini Uingereza Charlie Davis amesema uongozi wa klabu ya Chelsea endapo utashindwa kumaliza tatizo lilopo ndani ya klabu hiyo huenda mambo yakaendelea kwenda kombo klabuni hapo.
Charlie Davis akaendelea kubainisha wazi kwamba kwa asilimia kubwa mashabiki wengi wa klabu ya Chelsea pamoja na viongozi walitegemea huenda wangeokota point nyingi sana mwezi Novemba lakini hatua hiyo imeshindikana huku michezo ya mwezi Disemba ikionekana kuwa migumu zaidi ambapo klabu hiyo kuanzia mwishoni mwa juma hili itaanza kupambana na Spurs, kisha Arsenal na majuma mawili yajayo itapambana na Man Utd.
No comments:
Post a Comment