
Zikiwa zimepita siku mbili baada ya uongozi wa klabu ya Newcastle Utd kumtimua kazi aliekua meneja wa kikosi cha klabu hiyo Chris Hughton, uongozi wa The Magpies umetangaza kumtaja meneja mpya mwishoni mwa juma hili.
Wakati taratibu za uongozi wa klabu hiyo ya St Jame’s Park ukijiandaa kulianika wazi jina la meneja mpya, tayari kuna fununu zinaeleza kuwa huenda meneja huyo akawa ni Martin Jol toka nchini Uholanzi, Martin O’Neil kutoka jamuhuri ya Ireland, Alan Pardew ama Ray Wilkins wote kutoka nchini Uingereza.
Mameneja hao ambao kwa sasa wameachana na vilabu walivyokua wakivifundisha wanatajwa na vyombo mbali mbali vya habari nchini huku mashabiki wa Newcastle Utd wakipingana kwa kila mmoja kumtaka meneja anaemuona anafaa katika utaratibu wa kukinoa kikosi chao.
Wakati mameneja hao wakitajwa na kupewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya kukiongoza kikosi cha Newcastle Utd, mshambuliaji na nahodha wa zamani wa klabu hiyo Alan Shearer amekataa kata kata kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Shearer, mwenye umri wa miaka 40, ambae kwa mara ya kwanza alikabidhiwa kikosi cha The Magpies mwezi April 2009, na kujikuta akiipelekea klabu hiyo katika shimo la ligi daraja la kwanza amevieleza vyombo vya habari kwamba kwa sasa hayupo tayari kuwania nafasi hiyo lakini akatoa ahadi ya kumsaidia kimawazo yule atakaefanikiwa kuchukua nafasi ya Chris Hughton.
No comments:
Post a Comment