
Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger amesema inawalazimu kusubiri vipimo ambavyo vitawawezesha kwa lengo la kujua hali ya beki wa kushoto wa kikosi chake Kieran Gibbs ambae jana aliumia kifundo cha mguu alipokua kwenye haka heka za kuitetea klabu yake.
Wenger amesema kwa sasa hawezi kusema lolote juu ya hali ya beki huyo lakini akakiri kitendo cha kuumia kwa mchezaji huyo na kurejea katika benchi la majeruhi kimemuumiza sana.
Hata hivyo amemtakia kila la kheri Kieran Gibbs ili aweze kurudi haraka uwanjani na kuendelea na shughuli za kuitumikia klabu yake ambayo msimu huu imepania kufanya makubwa kwenye michuano wanayoshiriki.
Licha ya kumtakia kheri pia ametangaza kumuondoa kwenye kikosi cha klabu ya Arsenal ambacho mwanzoni mwa juma lijalo kitaifunga safari kuelekea Old Trafford kupambana na mashetani wekundu Man Utd.
Wakati huo huo mzee huyo wa kifaransa ameonyesha kufurahishwa na hatua ya kikosi chake kufanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja mbele ya Partizan Belgrade hapo jana.
Amesema kubwa lililo mbele yake kwa sasa ni kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya hatua inayofuata baada ya kumaliza katika nafasi ya pili ya kundi la nane ambalo linaongozwa na Shakter Doneski.
Kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo, Arsenal huenda wakakutana na vigogo vya soka barani humo ambavyo vimelamaliza katika nafasi ya kwanza katika makundi yao huku Barcelona wakitajwa sana huenda wakacheza na washika bunduki hao wa Ashaburton Grove.
Hata hivyo Arsene Wenger amethibitisha hadharani kutoihofia klabu yoyote watakayokutana nayo katika hatua ya 16 bora huku akikiria Barcelona wana nafasi ya kipekee katika michuano hiyo mikubwa katika ngazi ya vilabu barani ulaya.
Kwa upande wake mchezaji wa zamani wa klabu ya Arsenal Chalie Adam amezungumzia harakati za klabu ya Arsenal kuwa katika hati hati ya kukutana na vilabu nguli barani ulaya ambapo amesema anaamini klabu hiyo inaweza kuendelea kusonga mbele endapo itajipanga uzuri.
Amesema kikosi cha Arsenal kwa sasa sio kibaya bali kinahitaji kuongezewa nguvu ya baadhi ya wachezaji ambao watatakiwa kusajiliwa kupitia usajili wa dirisha dogo ambao utaanza mwanzoni mwa januari na kumalizika mwishoni mwa mwezi huo mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment