Hatimae ndoto za mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Togo Emmanuel Sheyi Adebayor za kutaka kuondoka City Of Manchester zimetimia kufuatia uongozi wa klabu yake ya Manchester City kukubali kumtoa kwa mkopo katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Adebayor ambae kwa kipindi kirefu alikua akiota ndoto ya kuondoka Man city baada ya kuchoshwa na mazingira ya kukaa benchi kila kukicha amefanikiwa kuondoka klabuni hapo na kujiunga na mabingwa wa zamani wa nchini Hispania pamoja na barani Ulaya Real Madrid ambao kwa sasa wapo chini wa meneja wa kimataifa toka nchini Ureno José Mário dos Santos Félix Mourinho.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 tayari ameshaondoka mjini Manchester na hii leo anatarajiwa kufanyiwa vipimio vya afya yake kabla ya kutambulishwa kwa waandishi wa habari.
Sababu kubwa ya kusajiliwa kwa Emmanuel Sheyi Adebayor huko Estadio Santiago Bernabéu ni kuziba nafasi iliyoachwa wazi na mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Argentina Gonzalo Gerardo Higuaín ambae atakuwa nje ya uwanja hadi mwezi April mwaka huu kwa sababu za kuwa majeruhi.
Baadhi ya vyombo vya habari vya nchini Hispania pamoja na Uingereza vimeeleza kwamba Emmanuel Sheyi Adebayor huenda akasajiliwa moja kwa moja na klabu ya Real Madrid mwishoni mwa msimu huu, na endapo dili hilo litakamilika uongozi wa The Merengues utatakiwa kulipa euro 15 million ambazo ni sawa na paund million 12.97.
No comments:
Post a Comment