Hatimae fununu za kutimuliwa kazi kwa meneja wa klabu ya West Ham utd Avram Grant hii leo zimemalizwa rasmi kufuatia uongozi wa klabu hiyo kutoa kauli inayohusiana na suala hilo.
Grant aliekua kikaangoni toka mwishoni mwa juma lililopita, amenusurika kutimuliwa kazi baada ya mabosi wake kutoa taarifa kupitia mtandao wa klabu ya West Ham Utd iliyosomeka kwamba bado wanaridhishwa na ufundishaji wa myahudi huyo.
Hata hivyo imeelezwa kwamba ushauri wa kutokutimuliwa kazi kwa Avram Grant umetolewa na alikua nahodha na kiungo wa klabu hiyo Julian Andrew Dicks ambae inasemekana kila mara amekua akifanya mazungumzo na uongozi wa The Hammers kujadili suala la kuondoka ama kubaki kwa meneja huyo mwenye umri wa miaka 55.
Sababu kubwa ya Julian Andrew Dicks kufanya hivyo mara kadhaa imekua ikielezwa kwamba endapo uongozi wa West ham utd ungefikia maamuzi ya kumuajiri meneja mwingine na kumfukuza Grant, kungekua na uwezekano wa kikosi cha The Hammers kupoteza muelekea na kufikia hatua ya kuporomoka daraja mwishoni mwa msimu huu.
Tayari meneja wa zamani wa klabu za Grantham Town , Shepshed Chaterhouse, Wycombe Wanderers, Norwich City, Leicester City, Celtic pamoja na Aston Villa Martin O'Neill alikua ameshaanza kuhusishwa na taarifa za kutaka kuchukua nafasi ya Avram Grant toka mwishoni mwa juma lililopita.
Ikumbukwe kuwa Avram Grant alikabidhiwa kikosi cha West Ham utd mwanzoni mwa msimu huu mara baada ya kutimuliwa kazi kwa mtaliano Gianfranco Zola mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kukinusuru kikosi cha The Hammers kurejea kwenye michuano ya ligi daraja la kwanza.
Mpaka sasa utawala wa Grant umeshuhudiwa kikosi cha West Ham Utd kikishuka dimbani mara 23 kucheza michezo ya ligi kuu ya soka nchini Uingereza na kufanikiwa kujikusanyia point 20.
No comments:
Post a Comment