Kiungo mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Argentina pamoja na klabu bingwa nchini Hispania Barcelona Lionel Andrés "Leo" Messi usiku wa kuamkia hii leo ametangazwa kuwa mchezaji bora wa dunia wa mwaka 2010.
Lionel Andrés "Leo" Messi ametangazwa kuendelea kushika nafasi hiyo kwa mara ya pili mfululizo, kwenye hafla ya utoaji tuzo za dunia iliyoandaliwa na shirikisho la soka duniani FIFA huko mjini Zurich nchini Uswiz yalipo makao makuu ya shirikisho hilo.
Messi, mwenye umri wa miaka 23, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo huku akiwabwaga wachezaji wenzake wa klabu ya Barcelona Andrés Iniesta Luján pamoja na Xavier Hernández i Creus.
Mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo bora ya dunia Messi aliwaeleza waandishi wa habari kwamba alishtushwa kwa jina lake kutajwa kuwa mshindi kwani alijua anapambana na wachezaji wenzake wenye uwezo mkubwa.
Katika hatua nyingine tuzo ya mchezaji bora wa kike imekwenda kwa mwana dada wa kibrazil Marta Vieira da Silva anaechezea klabu ya Santos ya nchini kwao.
Tuzo ya kocha bora wa kiume mwaka 2010 imechukuliwa na Jose Mourinho, huku tuzo ya kocha bora wa mwaka kwa upande wa wanawake imechukuliwa na kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Silvia Neid.
Hamit Altintop kiungo wa kimataifa toka nchini Uturuki na klabu ya Bayern Munich ya nchini Ujerumani yeye ametangazwa kuwa mfungaji wa bao bora la mwaka 2010, ambalo alilifunga kwenye mchezo wa kimataifa kati ya timu yake ya taifa dhidi ya Kazakhstan.
Nae askofu Desmond Tutu wa nchini Afrika kusini amepewa tuzo ya heshima na raisi wa shirikisho la soka duniani FIFA Sepp Blatter.
No comments:
Post a Comment