Fumbo la nani atakuwa mwenyeji wa fainali za mataifa bara la Afrika za mwaka 2015 na 2017 kati ya nchi za Afrika kusini pamoja na Morocco litafumbuliwa kesho baada ya kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho la soka barani Afrika CAF kitakachofanyika mjini Lubumbashi huko Jamuhuri ya kidemokrasia ya kongo.
Kikao hicho kinaketi hiyo kesho huku nchi hizo mbili zikiwa nchi pekee zilizowasilisha maombi ya kuwa wenyeji wa fainali hizo za mwaka 2015 ambapo hata hivyo kila nchi inatamani kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka huo na si mwaka 2017.
Raisi wa chama cha soka nchini Afrika Kusini Kirsten Nematandani tayari ameshatangaza azma yao ya kutaka kuona wanashinda nafasi ya kuandaa fainali za mwaka 2015 hivyo wana imani wajumbe wa CAF wataipa nafasi kubwa nchi yao kutimiza malengo waliyojiwekea.
Amesema hatua ya kuandaa fainali za mataifa ya Afrika kwa mwaka 2017 haitoleta chachu nzuri kwa nchi kama Afrika kusini ambayo bado ipo kwenye heka heka za kushuhudia fainali kubwa za soka zikiunguruma katika radhi ya nchi hizo mara baada ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010.
Kwa upande wao Morocco nao wanaitaka nafasi hiyo ya kuandaa fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2015, ili kuiwezesha nchi yao kujitangaza zaidi baada ya kufifia katika medani ya soka la barani Afrika sambamba na lile la ulimwengu mzima.
Yoyote atakaetangazwa kuwa mshindi katika fainali za mwaka 2015 hiyo kesho, atamfanya mpinzani wake kusubiri hadi mwaka 2017 ili aweze kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka huo.
Ikumbukwe kuwa fainali za mataifa ya bara la Afrika kwa mwaka 2012 zimepangwa kufanyika Equatorial Guinea kwa kushirikiana na nchi ya Gabon, zikifuatiwa na fainali za mwaka 2013 zitakazofanyika nchini Libya.
Kikao hicho cha kamati ya utendaji ya CAF kitafanyika mjini Lubumbashi saa chache kabla ya kuachezwa kwa mchezo wa kuwania ubingwa wa Super Cup ambapo mabingwa wa soka barani Afrika TP Mzembe watapambana na mabingwa wa kombe la shirikisho FUS Rabat.
No comments:
Post a Comment