Beki wa kulia wa klabu ya Man Utd Rafael Pereira da Silva ataukosa mchezo wa mwishoni mwa juma hili ambapo kikosi cha Mashetani wekundu kitaifunga safari hadi huko St Mary's Stadium kwenda kucheza na wenyeji wao Southampton katika mchezo wa hatua ya nne ya kombe la chama cha soka nchini Uingereza FA.
Rafael Pereira da Silva hatojumuishwa kikosini siku hiyo kufuatia maumivu makali yanayomuandama kichwani, kufuatia kugongana na mshambuliaji wa kimataifa toka nchini Uingereza na klabu ya Blackpool Marlon Anderson Harewood katika mchezo wa jana na kusababisha mchezo huo kusimamishwa zaidi ya dakika tatu.
Daktari aliemshughulikia Rafael, mwenye umri wa miaka 20, mara baada ya kutolewa uwanjani na machela huku akipumua kupitia mipira ya hewa ya Oxygen ameshauri mchezaji huyo kupumzishwa hadi hapo atakaporejea katika hali yake ya kawaida.
Hata hivyo vipimo vimeonyesha kuwa Rafael Pereira da Silva hakuathirika, zaidi ya kupata maumivu makali kichwani, hatua mbayo ilimfanya aruhusiwe hospitalini na kujiunga na kikosi cha Man Utd kilichorejea nyumbani mapema hii leo.
No comments:
Post a Comment