
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Rwanda Sellas Tetteh amesema kuna ulazima mkubwa sana kwa kikosi chake hii leo kuhakikisha kinapata ushindi katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya kundi la nne dhidi ya timu ya taifa ya Angola.
Sellas Tetteh amesema sababu kubwa ya kutimizwa kwa ulazima huo ni kutaka kubakisha heshima ndani ya michuano hiyo ambayo inayashirikisha mataifa bingwa barani Afrika kutoka kila ukanda wa bara hilo.
Amesema kimahesabu tayari wameshatupwa nje ya fainali hizo zinazofanyika nchini Sudan, hivyo hawana budi kuwafunga Angola kwa malengo ya kusaka heshima kwa taifa hilo pamoja na ukanda wa afrika mashariki na kati.
Kocha huyo wa kimataifa toka nchini Ghana ambae ana sifa kubwa barani Afrika kufuatia kuiwezesha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya taifa lake kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 2009 kwa kuibanjua timu ya taifa ya Brazil, pia ametoa sababu za kile kilichopelekea kufanya ovyo katika fainali za CHAN ambazo zinachezwa kwa mara ya pili toka zilipoanzishwa.
Amesema walikwenda nchini Sudan kusaka mafanikio ya kutwaa ubingwa wa fainali hizo lakini kwa bahati mbaya wamekutana na ushindani wa hali ya juu na hii leo wapo katika mchezo wa mwisho huku wakishikilia mkia wa kundi la nne kwa kutopata point hata moja.
No comments:
Post a Comment