
Mshambuliaji Lomana Trésor LuaLua amerejeshwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo inayojiandaa na mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za mataifa ya bara la Afrika mwaka 2012 utakaochezwa mwishoni mwa mwezi huu.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo Robert Nouzaret amesema amemrejesha kikosini Lomana Trésor LuaLua ambae kwa sasa anaitumikia klabu ya Omonoia Nicosia ya nchini Ugiriki amerejeshwa kufuatia kupona majeraha yaliyokua yakimkabili.
Amesema kurejea kwa mshambuliaji huyo kutaongeza chachu ya kusaka ushindi kwa wachezaji wake ambao watakua na kibarua kizito cha kuikabili timu ya taifa ya Mauritius mnamo March 27 huko mjini Kinshasa.
Kwa mara ya mwisho mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo mwaka 2009 katika harakati za kusaka nafasi ya fainali za mataifa ya bara la Afrika za mwaka 2010 zilizofanyika nchini Angola.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya kongo pia amemuita mshambuliaji wa klabu ya VfL Wolfsburg ya nchini Ujerumani Dieumerci Mbokani.
Mbokani, mwenye umri wa miaka 25 alitemwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo kilichopata matokeo ya sare dhidi ya Cameroon kufuatia sababu za utovu wa nidhamu lakini kwa hivi sasa kocha mkuu Nouzaret amesema anaamini mshambuliaji huyo atakua amebadilika kwa malengo ya kulisaidia taifa lake.
Mchezaji mwingine alierejeshwa kikosini ni kiungo wa klabu ya West Bromwich Albion ya nchini Uingereza Yousouf Mulumba, ambae anaungana na wachezaji sita wa klabu bingwa barani Afrika TP Mazembe Kaluyituka Dioko, Patou Kabangu, Bedi Mbeza pamoja na kipa Kidiaba Muteba.
Timu ya taifa ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo imepangwa katika kundi la tano lenye timu za Cameroon, Mauritius pamoja na Senegal.
No comments:
Post a Comment