
Beki wa zamani wa klabu za Valladolid, Real Madrid , Al Rayyan , Bolton Wanderers pamoja na timu ya taifa ya nchini Hispania, Fernando Ruiz Hierro ametangazwa kuwa mkurugenzi wa michezo wa klabu iliyopania kufanya mapinduzi ya soka nchini Hispania CF Malaga.
Fernando Ruiz Hierro ametangazwa kushika wadhifa huo huko La Rosaleda, ukiwa umepita mwezi mmoja baada ya kutangaza kujizulu nafasi ya mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la soka nchini Hispania ambapo akiwa katika nafasi hiyo alifanikiwa kulisaidia benchi la ufundi la timu ya taifa kutwaa ubingwa wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 zilizofanyika nchini Afrika kusini.
Uongozi wa klabu ya Malaga unaamini kwamba Hierro, atafikia malengo yaliyowekwa klabuni hapo ya kuhakikisha kikosi chao kinafanya vyema katika msimu mpya wa ligi ambao utaanza kuunguruma mwishoni mwa mwezi ujao.
Hata hivyo imeelezwa kwamba ukaribu uliopo kati ya Hierro pamoja na meneja mpya wa klabu ya CF Malaga, Manuel Pellegrini utachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya muda mfupi yaliyowekwa ambayo ni pamoja na kusajiliwa kwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
Mpaka sasa klabu hiyo iliyo katika pwani ya kusini mwa nchini Hispania imeshakamilisha usajili wa wachezaji wanane wenye uzoefu mkubwa ambao ni Ruud Van Nistelrooy, Joaquín Sánchez, Joris Mathijsen, Jeremy Toulalan, Nacho Monreal, Martín Demichelis, Sergio Sanchez pamoja Santi Cazorla.
No comments:
Post a Comment